December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Waziri ataka mifumo itumike kuweka taarifa sahihi

Na Joyce Kasiki,Dodoma

KATIBU Mkuu wizara ya maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameziagiza Mamlaka za Maji na Wakala wa Maji mijini na Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanatumia mifumo ya maji kwa weledi kwa kuweka takwimu sahihi na siyo takwimu za kupika.
Mhandisi Waziri ametoa kauli hiyo wakati akifunga kongamano la kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili ambalo lilienga kuimarisha usafi wa mazingira.

Amesema uwepo taarifa sahihi kwenye mifumo utawawezesha wadau na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kupata taarifa sahihi na kuzifanyia kazi bila kuwasiliana na mtaalam husika.
Amesema katika kongamano hilo wadau wamejifunza na kujafili mifumo ya taarifa za Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira ambayo ni Mfumo wa Uwasilishaji wa taarifa za Majisafi na Usafi wa mazingira (MAJIS) na Mfumo wa ufuatiliaji wa Taarifa za Usafi wa Mazingira huku akisema mifumonhiyo itumike vizuri na siyo kuweka takwimu za kupika.
“Maana yake mara nyingi tumeona mifumo inatusaidia ,lakini wakati mwingine wataalam wetu kule mnapika data ili muweze kuonekana mpo kwenye viwango vinavyohitajika,lakini mtu akija kwako katika uhalisia wakati mwingine unakuta wewe mwenyewe unabishana na data.”amesema Mhandisi Waziri
Aidha Katibu Mkuu huyo amewaagiza waandaaji wa Kongamano hilo kuhakikisha maagizo yaliyotolewa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko ,na maazimio waliyoyaazimia kuyawekea mpango kazi wa kuyatekeleza na wahusika wote walioanishwa watekeleze maagizo hayo kwa wakati.
Amesisitiza kuwasilishwa kwa utekelezaji wa maagizo hayo ofisi ya Dkt.Biteko na Ofisi ya Waziri Mkuu ,Bunge na Uratibu na Wizara ya Maji ili kufanya ufuatiliaji.
Aidha amesema, uwepo wa Kongamano la kitaifa la usafi wa Mazingira linaenda kupunguza changamoto za magonjwa hasa ya mlipuko kama kipindupindu huku akiigiza EWURA kuhakikisha inaendelea kufanya makongamano mengine ya usafi wa mazingira.
“Naipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kwa kuandaa kongamano hili maana Wizara ya Maji suala la usafi wa mazingira limekuwa likitupa changamoto hasa wakati wa mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu ,lawama nyingi zimekuwa zkionesha milipuko hutokea kutokana na Wizara ya maji kutoa maji ambayo huenda siyo salama.”amesema Mhandisi Waziri
Ameongeza kuwa “Kwa hiyo kwa kongamano hili linaenda kusaidia kupunguza lawama na changamoto za magonjwa hasa ya mlipuko
Vile vile amesema Wizara ya Maji imechukua na inaenda kufanyia kazi maoni ya wadau yaliyotolewa katika kongamano hilo kwenye mabadiliko ya Sera ya Maji ambayo ipo kwenye mchakato wa kufanyiwa mabadiliko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt.James Andilile amesema mada mbalimbali ziliwasilishwa kwenye kongamano hilo ikiwa ni pamoja na mada ya
mifumo ya uhifadhi wa takwimu za usafi wa mazingira,Mpango jumuishi wa masuala ya usafi wa mazingira lakini pia wamepitia kwa undani miongozo iliyozinduliwa katika kongamanonhilo ili kujenga uelewa wa pamoja.
Amesema mada nyingine zilizowasilishwa ni kuhusu Changamoto,mafanikio na mapendekezo mbalimbali kuhusiana na usafi wa mazingira ,lakini pia wameptia habari ya fedha ya maji iliyopo ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu usafi wa mazingira .
“Baada ya mawasislisho na mijadala hiyo EWURA inaamini itakuwa ni chachu yabkusogeza mbele masuala ya uboreshaji wa usafi wa mazingira”amesema Dkt.Andilile
Aidha amesema wameyachukua maagizo ya Dkt.Biteko lakini pia wamekuja na maazimio 15 ambayo yatawawezesha kujipima na kuona watakuwa wamepiga hatua kiasi gani watakapokutana tena huku akisema kongamano hilo litakuwa endelevu.
Wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo pamoja na mambo mengine ,Dkt.Biteko aliwaagiza wadau wanaohusika na udhibiti na utoaji wa huduma ya usafi wa mazingira ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA),Wizara,Mamlaka za Serikali za Mitaa,sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano hasa katika utoaji wa huduma hiyo ili kulinda na kuimarisha afya za wananchi.