Na Saida Bawazir, Timesmajira Online
UNAPOZUNGUMZIA Maji ni kimiminika ambacho kiini cha uhai wowote duniani na pia kiini cha utamaduni wa binadamu. Hakuna mtu anayeweza kuishi bila maji kwa sababu asilimia 50 – 65 za mwili wa mwanadamu ni maji.
Hata miili ya mimea na wanyama kwa kiasi kikubwa ni maji. Pia katika dunia maji yamechukua karibu robo tatu ya eneo lake lote (71.11%). Kwa hiyo maji ni kitu cha msingi sana.
Maji yana matumizi mengi nyumbani na katika uchumi: nyumbani maji hutumika katika kunywa, kuogea, kuoshea vitu na vyombo mbalimbali; kiuchumi maji yanatumika viwandani, kwa mfano kupoozea au kuoshea mashine, pia maji hutumika katika usafiri, kama vile meli za mizigo, za abiria na vinginevyo.
Katika matumizi hayo pengine watu hutumia vibaya maji na vyanzo vyake ambavyo ni muhimu vitunzwe kwa kuwa tukiharibu vyanzo hivyo twaweza kuleta hali ya jangwa katika eneo hilo.
Maji ni muhimu sana kwa afya ya mwanadamu. Maji yanasaidia kuondoa sumu mwilini, kusaidia mmeng’enyo wa chakula, na kuboresha afya ya ngozi, husaidia kuepuka presha ya kushuka na afya kwa ujumla.
Ni jambo la kufurahisha sana kwa wakazi wa maeneo ya Kimara na viunga vyake kupata maji ya DAWASA. Kimara ni moja ya maeneo ndani ya jiji la Dar es Salaam ambako ilikuwa ukimuuliza hata mtoto mdogo kero ya eneo hilo atakwambia maji.
Kukosekana kwa maji eneo la Kimara pamoja na sababu nyingine lakini kulikuwa na mikono ya baadhi ya watu wenye nguvu waliogeuza mradi wa kuuza maji kwa magari kuwa njia yao kuu ya kujipatia mapesa. Hali hiyo ikafanya suala la kupata maji ya bomba kuwa kilio cha miaka nenda rudi.
Shukrani za pekee zimfikie Diwani wa Kata ya Kimara Mhandisi Ismail Mvungi ambaye hivi karibuni amefanya mkutano wa hadhara mahsusi kwa kutoa taarifa ya Maendeleo ya Miradi ndani ya kata hiyo.
Miradi hiyo iliyofanyika toka mwaka 2o20-2024. Mkutano huo umefanyika katika eneo la Stendi ya Noah lililopo katika Mtaa wa Golani, Kata ya Kimara Wilaya ya Ubungo.
Katika mkutano huo walialikwa wataalamu kutoka Dawasa, DMDP, TARURA pamoja na Viongozi wa Kiserikali, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya Kata.
Diwani Mvungi anasema, ameamua kuandaa mkutano huo na kuwakaribisha wataalamu ili watoe majibu kuhusu changamoto ya maji inayowakabili wananchi wake ili zipate utatuzi.
“Niwapongeze wananchi wote wote ambao mmefika katika mkutano huu kwaajili ya kutoa taarifa zinazohusiana na maendeleo yanayofanyika ndani ya Kata ya Kimara,
“Naomba muwe tayari kupokea taarifa hizo lakini nitawapa nafasi za kusikiliza kero zenu ambapo zenye majibu tutawapa majibu na ambazo hazina tutazibeba kwaajili ya kuzipeleka sehemu husika na kuzishughulikia,” anasema Diwani Mvungi.
Akizungumzia Miundombinu ya Maji, Mhandisi Mvungi diwani wa kata hiyo ya Kimara aliwakaribisha wananchi kuelezea kero zao ambapo kero kuu ilikuwa ni kukosekana kwa maji hasa kipindi cha mvua.
Lakini pia, kucheleweshwa kupatikana kwa namba ya malipo ‘Control Number’ kwa wateja wapya ambao wanahitaji kupatiwa huduma ya kuunganishiwa maji.
Anasema, mbali na hivyo pia kuchelewa kufungiwa kupatiwa huduma hiyo ya maji mara baada ya kufanyika kwa malipo kwa mteja mpya ambapo inaweza kufikia hata miezi sita mteja akisubiri kuunganishiwa maji.
Mhandisi Mvungi, alimtaka mkandarasi toka DAWASA atoe ufafanuzi juu ya kero ya ukosekanaji wa maji kwa wananchi kutokana na baadhi ya mabomba ya maji kukatika wakati ujenzi wa barabara ukiendelea katika maeneo ya Golani.
Pia, atoe taarifa juu ya kituo kinachojengwa kwa Mashaka ili wananchi wawe na uwelewa na wafahamu kituo hicho kinahusiana na nini.
Akijibu kero za wananchi kuhusu miundombinu ya Maji, Mkandarasi Adamu Bariki Massam Kutoka DAWASA anasema Changamoto ya ukosefu wa maji hutokana na kuachia bomba kubwa lililopita kutoka Kimara na kuelekea kwa Kitila Mkumbo kupasuka.
“Hali hii husababishwa na eneo lililopita bomba hilo kuwa korofi, hivyo inapotokea bomba hilo limeachia huwa DAWASA tunafunga maji katika njia kubwa ili kuweza kufanya ukarabati wa bomba hilo na huduma za maji kurudi kama kawaida japo maji hayo hurudi kwa taratibu sana katika mfumo wake.
“Mkakati uliopo ni kubadilisha bomba hilo kutoka katika plastic ‘pvc’ na kuweka bomba la chuma ili tuweke kitu imara na chenye kudumu kwa muda mrefu,” anasema Mkandarasi Massam.
Anasema, tatizo lingine ni uhamishaji wa miundombinu kutokana na ujenzi unaotaka kuanza kutoka Kimara kuelekea Bonyokwa tayari DAWASA imeshawasilisha bajeti kwa TANROAD na hali inaendelea vizuri, hivyo wakati kazi ya kuhamisha miundombinu hiyo utaanza kabla ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza rasmi.
Kutokana na mpango mkakati walionao muda si mrefu hakuna mwananchi atakayekosa maji katika kipindi hicho cha ujenzi utakapokuwa unaendelea.
Vilevile Mkandarasi huyo amezungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji toka Bonyokwa hadi Kinyerezi, anasema Dawasa ilifanya utafiti wa kuangalia ni kwa namna gani changamoto hiyo inaweza kutatulia.
Mkandarasi Massam anasema, tatizo la upatakinaji wa maji wa maeneo hayo umeanzia kwa Kichwa na ndio maana wamejenga kituo hicho.
“Kwa kichwa ndio eneo maji yanapoishia kwamaana hiyo kituo hiki kitakuwa kinahifadhi maji kisha kuyasukuma na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali kuanzia ndani ya Kata ya Kimara,” anasema.
Kuhusu suala la uchelewaji wa kupatiwa namba ya malipo ‘control number’ Mhandisi Massam anasema hali hiyo imetokana na mfumo lakini wataalamu wanalishughulikia tatizo hilo na ndani ya mwezi huu namba hizo za malipo zitaanza kutolewa.
Anasema, kwa upande wa ucheleweaji wa kufungiwa maji changamoto ipo kwa upande wa kitengo cha manunuzi kuchelewa kupata vifaa.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia