November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi apongezwa kuunganisha wanawake

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Kyela

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amempongeza Naibu Waziri wa Maji (Mb) Mhandisi Maryprisca Mahundi kwa namna anavyojitoa katika kuwaunganisha wanawake na kuwawezesha kiuchumi ili waweze kuondokana na hali ya kuwa na tegemezi.

Mwalunenge amesema hayo Desemba 22,2023 wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Mbeya (UWT) ulioandaliwa na Mhandisi Mahundi ambao umefanyika katika ufukwe wa Matema.

“Mnaona Mhandisi Mahundi anavyounganisha wanawake,kuwezesha kiuchumi na kuwaweka pamoja,ameenda nje zaidi na kuwawezesha kiuchumi wanawake ambao si wapiga kura ,haya anayofanya Mbunge huyu na wabunge wengine waige mfano huu,”amesema Mwenyekiti huyo.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa Mbeya amesema kuwa Ubunge ni uwakilishi lazima uwasababishie wenzio waone thamani na faida ya kuwa na Mbunge na ifike mahali mtu akitaka kugombea.

Aidha Mhandisi Mahundi ameongeza kuwa kufanikiwa wanawake inawezekana kwani vyote vipo mikononi mwao na kusema kuwa wakate shauri na kudhamiria kikubwa kujenga nia ya pamoja.

“Wanawake tukidhamiria tunaweza sana hivyo tujitume kufanya shughuli mbalimbali za kujiongezea uchumi na kufanya makubwa ya kushangaza dunia na ukawa msaada kwa familia nzima “amesema.

Mhandisi Mahundi amewakutanisha wanawake wa Wilaya Saba za Mkoa wa Mbeya lengo likiwa ni kuwawezesha kiuchumi zaidi,kuwasisitiza na kushikamana ili kumpa kura za kishindo Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwezesha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwa upande wake Diwani Viti Maalum Kata ya Makongolosi wilayani Chunya mkoani Mbeya,Sophia Mwanauta amesema kuwa wanamshukuru Mhandisi Mahundi jinsi alivyo karibu na wanawake wa Mkoa wa Mbeya bila kujali wapiga kura wake amekugusa mama lishe wa hali ya chini ,vijana,wazee.

“Leo yupo na wanawake wa UWT Mkoa wa Mbeya ambapo amewaongeza mitaji ili tuweze kujiinuaa kiuchumi zaidi hii mitaji sio mara kwanza amekuwa akifanya mara kwa mara tunamshukuru sana kwani wengi wetu ametuheshimisha na hii ni zawadi kwetu kwa wanawake wa Mkoa huu,”amesema Mwanauta.