December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi alitaka Jeshi la polisi kuendelea kutoa elimu usalama barabarani

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

NAIBU Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhandisi Maryprisca Mahundi amelitaka jeshi la polisi mkoani Mbeya kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa barabara hasa madereva na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya madereva wanaokiuka sheria hizo na kuhatarisha usalama.

Mhandisi Mahundi amesema hayo leo Disemba 07, 2024 wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika katika Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya.

“Jeshi la polisi bado mna wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa elimu ya usalama barabarani inaendelea kutolewa hasa kipindi hichi cha kuelekea sikukuu,lakini sheria ichukue mkondo wake katika kuwathibiti madereva wazembe”amesema Mhandisi Mahundi .

Aidha Mhandisi Mahundi amewataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na makosa ya kibinadamu ikiwemo uzembe.

Aidha,Mahundi amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaotumia Bajaji na Pikipiki maarufu kama Bodaboda kupakia wanafunzi kupita kiasi na kuhatarisha usalama wa watoto wao na kuwataka kujari maisha ya watoto wao.

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amesema kuwa, kilele cha maadhimisho hayo kunafungua kurasa mpya kwa Jeshi la Polisi kwani wanakwenda kuendesha oparesheni kali kwa watumiaji wa vyombo vya moto .

Kamanda Kuzaga amesema kuwa oparesheni hiyo itakuwa Kwa vyombo vya moto ambavyo havijakaguliwa na kuwataka madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha vyombo vyao vinakaguliwa na kubandikwa stika ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu wa Polisi ,Notker Kilewa amesema katika wiki ya nenda kwa usalama barabarani walijikita kufanya shughuli mbalimbali za kuelimisha jamii masuala ya usalama barabarani, kutembelea vituo vya mabasi na kutoa elimu kwa madereva, wamiliki, mawakala na abiria, kutembelea na kukagua maeneo tete ya Iwambi, Mlima Nyoka na barabara ya Chunya.

Ameongeza kuwa, wamefanya ukaguzi wa Magari 1,126 katika eneo la Mlima Nyoka hadi Pipeline kabla ya magari kushuka mlima ambapo magari 28 yalifungiwa kutokana na ubovu uliokithiri.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mhandisi Rajabu Ghuliku amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na wadau wengine wa usalama katika kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani na kuongeza kuwa wao kwa kushirikiana na Chuo cha VETA wataendelea kuandaa kozi mbalimbali za muda mfupi kwa ajili ya kuwakumbusha na kuwajengea uwezo madereva na kuwafanya kuwa mahiri katika fani ya udereva ili kuepuka ajali zisizo kuwa za lazima.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Serikali, dini, kimila, mabalozi wa usalama barabarani (RSA), Madereva wa vyombo vya moto, wadau wa usalama barabarani, wanafunzi na wananchi huku yakibeba kauli mbiu inayosema “ENDESHA SALAMA, UFIKE SALAMA”