March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Kalimbaga  Rais mpya Chama cha Mifuko ya Barabara Afrika(ARMFA)

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Monrovia Liberia 

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko  wa Barabara Tanzania(RBF), Mhandisi Rashid Selemani Kalimbaga,amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA).

 Mhandisi Kalimbaga,amechaguliwa Novemba 20,2025,siku ya nne ya mkutano mkuu wa 22 wa mwaka wa shirika hilo unaofanyika  mjini Monrovia nchini Liberia,ambaye anachukua nafasi kutoka kwa Essaie Moussa Aubin wa Cameroon  anayemaliza muda wake huku akitarajia kudumu katika nafasi hiyo kwa miaka miwili(2025-2027).

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania(RFB),Mhandisi Rashid Selemani Kalimbaga wa pili kulia akiwa na viongozi wengine katika mkutano mkuu wa 22 wa mwaka wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA),ambao umechagua kuwa Rais wa chama hicho

 Ambapo kuchaguliwa kwa Mhandisi  Kalimbaga,kunaashiria awamu mpya ya uongozi kwa baraza la bara lenye jukumu la kuratibu na kuimarisha ufadhili wa matengenezo ya barabara kote barani Afrika.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mhandisi Kalimbaga amesema, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kuboresha mifumo ya kukusanya fedha za matengenezo,kwani nchi nyingi zinaendelea kutatizika na ukosefu wa fedha za kutunza barabara. 

“Tuna tatizo la kupata fedha za kutosha za matengenezo,lazima tuweke utaratibu wa kuhakikisha kuwa tunaongeza fedha za barabara ili tuweze kutunza barabara zetu kwa ufanisi,”amesema Mhandisi Kalimbaga.

Amesema kuimarisha muonekano, usajili wa ARMFA na Umoja wa Afrika kutasalia kuwa muhimu katika ajenda yake, kwa kuzingatia juhudi zilizoanzishwa na mtangulizi wake. 

“Tunapaswa kuendeleza juhudi zote za kufanya chama kijulikane na kusajiliwa vyema katika AU, ili tuweze kutimiza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi.Bila barabara, hakuna maendeleo hivyo ni jukumu letu kuhakikisha  mitandao ya barabara kote Afrika inapitika ili watu waweze kupata huduma na kukuza  uchumi,”amesema Mhandisi Kalimbaga.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania(RFB),Mhandisi Rashid Selemani Kalimbaga,ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA

Sanjari na hayo Mhandisi Kalimbaga, ameleza kuwa anatarajia kuungwa mkono na uongozi wake wa kitaifa anapotekeleza majukumu ya  Bara.Huku akitoa  wito kwa viongozi wenzake wa ARMFA waliochaguliwa pamoja naye, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuimarisha na kusaidia kutatua changamoto za taasisi hiyo.

 Pia ametumia fursa hiyo  kuipongeza  Liberia, mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu, kwa ukarimu,uboreshaji wa miundombinu na juhudi zinazoendelea za kupanua ufikiaji wa barabara nchini kote.