April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhagama ahimiza matumizi ya Tehama katika utumishi wa Umma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amewataka wakuu wa Vitengo vya Tehama Serikalini kusimamia matumizi ya mifumo ya Tehama ili kuongeza tija katika Utumishi wa Umma.

Mhagama ameyasema hayo leo wakati akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha wakuu wa Idara za Tehama Serikalini chenye lengo la kujadili uzingatiaji wa sheria ,Kanuni taratibu, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za umma.

“Serikali  Mtandao siyo teknolojia kama inavyochukuliwa na wengi,  ni matumizi ya TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku katika Taasisi za Umma pamoja kutoa huduma kwa Umma zenye tija.”amesema Mhagama na kuongeza kuwa

“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 kwa pamoja zinatambua nafasi ya Tehama katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza haja ya ongezeko la matumizi yake katika utendaji wa shughuli za Serikali na utoaji huduma kwa Umma.” 

Kwa mujibu wa Mhagama ili kuhakikisha Tehama inatoa mchango chanya katika uendeshaji na usimamizi wa majukumu ya Serikali, jitihada mbalimbali zimefanyika na mafanikio yamepatikana katika maeneo ya Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo, Usimamizi, Miundombinu, Mifumo tumizi na Shirikishi na Huduma za Serikali Mtandao.

“Yameonekana  manufaa ya kusanifu, kutengeneza, kusimika na kuendesha mifumo mhimili na tumizi ya kimkakati na kisekta kwa kutumia wataalamu wa ndani kutoka katika taasisi zenu na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao. “amesema

Hata hivyo Mhagama amesema  pamoja na mafanikio yaliyopatikana , lakini eneo hilo bado linakabiliwa na changamoto za kiutekelezaji, zikiwemo kutoshabihiana kati ya taratibu za utendaji kazi Serikalini  na teknolojia inayotumika,kutopatikana thamani halisi ya fedha zinazotumika kwenye miradi ya Tehama Serikalini na kuwepo kwa mifumo isiyowasiliana au kubadilishana taarifa (ndani ya taasisi, na kati ya taasisi na taasisi).

Vile vile amesema,urudufu wa mifumo miongoni mwa Taasisi za Serikali yenye viwango na gharama tofauti zisizo na uhalisia, Huduma za Serikali Mtandao kutowafikia wananchi wote hasa wa vijijini na kuongezeka kwa matishio ya usalama wa taarifa katika mifumo na Miundombinu ya Tehama.

Mhagama amesema  kuwa, uwezo wa kutatua changamoto hizo upo ndani ya taasisi za watendaji hao.

Ametumia nafasi hiyo kuwaagiza kuanza kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kuhakikisha sheria, kanuni, viwango, na Miongozo ya Serikali Mtandao  inazingatiwa na kufuatwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA Mhandisi Benedict Ndomba

Awali akitoa maelezo ya Mamlaka ya Serikali Mtandao ,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo  Mhandisi Benedict Ndomba  amesema lengo la matumizi ya Tehama ni kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi ili wananchi wapate huduma za Serikali kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.

Aidha amesema,pamoja na jitihada hizo, kumekuwepo na baadhi ya Taasisi za Umma zisizozingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao inayoelekeza matumizi sahihi na salama ya Tehama hivyo kusababisha kuwepo kwa urudufu wa Mifumo, Mifumo isiyozungumza na Miradi ya Tehama ambayo haijaidhinishwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Amesema hali hiyo  inaweza kupelekea Serikali kutopata tija kwenye uwekezaji unaofanyika kwenye Tehama.

Vile vile amesema, ipo pia changamoto ya upungufu wa watalaamu wa Tehama wenye uwezo na ujuzi wa kutosha, na uratibu hafifu wa shughuli za Tehama ndani ya Sekta mbalimbali na ndani ya Taasisi za Serikali.  

“Katika kukabiliana na changamoto hizo, Mamlaka imeendelea kuhimiza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma,hii ni  pamoja na kufanya kaguzi za Mifumo, kufuatilia Usalama wa mtandao na kushughulikia viashiria vya Matishio ya Kiusalama Mtandaoni, kutoa msaada wa kiufundi na kufanya utafiti na Mafunzo kuhusu Serikali Mtandao,”amesema Mkurugenzi huyo

Aidha amesema, Mamlaka imeandaa mpango kazi kwa ajili ya Mifumo yote ya Tehama  Serikalini kuweza kubadilishana Taarifa kupitia Mfumo wa GovESB.