December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhagama aeleza mafanikio wizara yake mwaka mmoja wa Rais Samia

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama ametaja mafanikio ya wizara hiyo katika mwaka mmoja wa uongozi Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo suala zima katika matumizi ya mifumo ya Tehama chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao(eGA) na hivyo kurahisisha utendaji kazi katika utumishi wa umma kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari Mtumba jijini hapa kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo Mhagama amesema, Mafanikio haya yanatokana na azma ya Mhe. Rais ya kutaka kuujenga utumishi wa umma wenye tija katika maendeleo ya Taifa.

Amesema,mafanikio yaliyopatikana katika eneo hilo ni pamoja na kuendelea kujenga mifumo imara ya utunzaji wa kumbukumbu, nyaraka na amali za taifa pamoja na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa siri za Serikali kwa Viongozi na Watumishi wa Umma.

“Pamoja na maelekezo ambayo Mhe.Rais amekuwa akiyatoa katika Ofisi hii ambapo tumepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali likiwemo la Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA inayohusu uendeshaji wa Serikali wa kila siku, kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma na kuimarisha maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwa kutumia mifumo.”amesema Mhagama na kuongeza kuwa

“Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na kuzingatia dhamira aliyoionyesha Mhe. Rais wakati akihutubia Bunge la 12 kwa mara ya kwanza zimedhihirisha kasi ya kiwango cha juu cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021-2026) .”

Kwa mujibu wa Waziri huyo, katika kipindi hicho wizara yake imefanikiwa kusimamia mageuzi katika Utumishi wa Umma katika kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara na imefanikiwa kuangalia upya Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi (OPRAS) ili kupata mfumo sahihi wa usimamizi wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini .

Aidha Waziri huyo amesema,katika kipindi  cha mwaka mmoja madarakani cha Rais  Samia kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kuanza kujenga Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) .

Amesema ,mfumo huo utaondoa changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendajikazi wa watumishi hali iliyoleta hisia za kupendeleana au kuoneana na kutokutumika kwa matokeo ya utendajikazi katika kufanya maamuzi ya kiutumishi.

Pia utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji wa watumishi,utaweka mifumo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi wa watumishi kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa na yanayopimika.

Aidha mfumo huu pia utahamasisha uwajibikaji wa hiari na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa watumishi.

Ofisi ya Rais Menejementi ya Utumishi wa Umma imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA inayohusu uendeshaji wa Serikali wa kila siku na kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma .

Amesema ofisi hiyo imejenga  Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI kwa lengo la kuwawezesha watumishi na wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi na Utawala.

”Mfumo huu pia unamuwezesha Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kuongea moja kwa moja na mlalamikaji ili kujua ni kwa namna gani tatizo lake limefanyiwa kazi na kuchukua hatua stahiki.”amesisitiza Mhagama

Katika hatua nyingine Mhagama amesema katika kipindi hicho mwaka mmoja chini ya uongozi wa Rais Samia wizara yake imeendelea kuhuisha sera na kanuni za Utumishi wa Umma ili ziendane na mazingira na mahitaji ya sasa ya ujenzi wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Pia imefanikiwa kujenga uwezo wa Viongozi na Watumishi wa Umma ili waweze kuwatumikia wananchi kikamilifu na kubuni mbinu na mikakati ya kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapata makazi bora kwa gharama nafuu.

Akifafanua zaidi Mhagama amesema,katika eneo la kusimamia mageuzi katika Utumishi wa Umma na kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara,  Rais Samia kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ametekeleza mambo mablimbali ikiwemo kuwapandisha vyeo/madaraja Watumishi 190,781 wenye sifa stahiki.

Aidha jumla ya shilingi bilioni 39,649,988, 204 na kazi inaendelea,kulipa madeni ya mishahara ya Watumishi wa Umma 65,394 yenye thamani ya shilingi bilioni 91,087,826,006.34 na kuwabadilisha kada Watumishi wa Umma 19,386 na kuwalipa mishahara mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 1,330,306,572.

Mhagama amesema katika kipinid hicho vimetolewa vibali 12,336 vya ajira mpya na mbadala ambapo jumla ya shilingi bilioni 7.761 zimelipwa,kuwapunguzia kodi watumishi wa umma kutoka asilimia 9 mpaka 8.

Akizungumza kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mhagama amesema,Ofisi ya  Rais Utawala Bora kupitia TAKUKURU na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imefanikiwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla.

”Vile vile hali ya maadili ya viongozi imeimarika  na kupata mafanikio lukuki yakiwemo Taarifa ya utafiti iliyofanywa na Transparency International  ya mwaka 2021 katika kiashiria cha Corruption Perception Index (CPI) kinaonesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwa kupata alama 39 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180, ikiwa imepanda kwa nafasi 7 ikilinganishwa na nafasi ya 94 ya mwaka 2020.”amesema na kuongeza kuwa

” Nchi yetu imeshika nafasi ya pili kwa Ukanda wa Afrika Mashariki katika kiashiria hicho cha CPI.”amesema Mhagama

Vile vile amesema Ofisi ya Rais Utawala Bora kupitia TAKUKURU imefanikiwa kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo 1297 yenye thamani ya shilingi trilioni 5.094 katika sekta za Afya, Elimu, Fedha, Nishati, Ujenzi, Maji, Uvuvi, Maliasili na sekta ya Kilimo. Matokeo ya ufuatiliaji huo yalibainisha miradi 133 yenye thamani ya shilingi bilioni 55.6 kuwa na kasoro mbalimbali na kuanzishiwa uchunguzi.

Aidha pamoja na mambo mengine  TAKUKURU kupitia operesheni zake mbalimbali imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi 3.017.