July 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgunda: Nakubali kubeba lawama

Na Mwandishi Wetu

KOCHA mkuu wa timu ya Coastal Union amekubali kubeba mzigo wa lawama baada ya kupoteza kwa goli 3-0 mchezo wao wa juzi uliochezwa kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga.

Kupoteza mchezo huo ni mwendelezo wa matokea mabaya waliyoanza nayo msimu huu yakiwaweka nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza mechi tatu.

Mgunda amesema kuwa, kama mwalimu anabeba lawama kwakua makosa yamefanywa na wachezaji wake.

Ukiangalia katika mchezo huo, kosa lililowagharimu na kupatikana magoli yote matatu ni la aina moja kwani baada ya Yanga kupata goli la kwanza aliwaambia wachezaji wake eneo walilotakiwa kujichunga nalo lakini bado walirudia kosa lile lile.

“Kosa la aina moja lililofanywa na mabeki wangu wa kati limetugharimu kufungwa goli zote tatu, nimehangaika sana kutafuta mawasiliano hadi sasa sauti imenikauka nao lakini bado walirudia kosa lile na kufanya wapinzani wetu kuongeza magoli hivyo kama mwalimu lawama zote nazibeba mimi kwani unapocheza na wachezaji walio vizuri kichwani na wakigundua unafanya makosa ya kujirudia rudia basi ni lazima wakuadhibu, ” amesema kocha huyo.

Amesema kuwa, siku zote mpira ni mchezo wa makosa hivyo anayapotea matokeo hayo ingawa haikuwa nzuri kwao kwani yanazidi kuwaweka pabaya.

Kocha huyo pia, licha ya makosa hayo lakini pia kuna mazuri mengi yamefanywa na wachezaji wake hivyo anarudi kujipanga na kusahihisha makosa yao kabla ya mchezo wao ujao dhidi ya KMC utakaochezwa Oktoba 14 katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.