March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea wa ACT-Wazalendo atoa wito wa uongozi wenye maono Zanzibar

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema ukosefu wa utawala wenye maono na dira thabiti ndio chanzo kikuu cha Zanzibar kubaki katika umasikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi za kiuchumi.

Akihutubia wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni, katika Jimbo la Chonga Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini PEMBA,Othman amesema Zanzibar imejaliwa fursa kubwa za kiutalii, kilimo cha baharini na biashara za kimataifa, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kutokuwepo kwa viongozi wenye mipango ya maendeleo ya muda mrefu na inayotekelezeka.

“Zanzibar haikupungukiwa na rasilimali, tatizo letu ni ukosefu wa uongozi wenye dira. Tunahitaji viongozi wanaoweka mbele maslahi ya wananchi na si maslahi ya kisiasa binafsi,” alisema.Othman alibainisha kuwa chama cha ACT-Wazalendo kimejipanga kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo kuboresha huduma za afya, elimu na ajira kwa vijana.

Ameongeza kuwa kipaumbele cha chama chake ni kujenga uchumi shirikishi utakaonufaisha wananchi wote badala ya wachache.Aidha, aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao na kufanya maamuzi ya kuleta mabadiliko, akisisitiza kuwa chama chake kimeweka wazi mipango ya maendeleo yenye kujali utu na ustawi wa wananchi.