March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Urais ACT Wazalendo: Tutabadilisha Muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameapa kwamba serikali yake itafanya mabadiliko makubwa ya muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kulinda maslahi ya leo na vizazi vijavyo kuepuka maafa yasiokua na lazima ambayo yamekua yakitolea kila baada ya miaka Mitano ya Uchaguzi.

Akizungumza na wazee mashuhuri wa Shehia ya Pujini, Wilaya ya Chake Chake, Othman alisema tume ya sasa imekuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa visiwani kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa haki na badala yake kujigeuza kuwa ngao ya maslahi ya CCM.

Amesema kwa mara kadhaa wamekua wakishauri na kujishusha kwa watawala wakidai mabadiliko ya muundo wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuepusha maafa na majanga ambayo Zanzibar imekua ikikabikiana nayo kila baada miaka mitano ya uchaguzi.

Othman ametolea mfano uchaguzi wa mwaka 2020 alisema watu 21 waliuwawa na vyombo vya Dola katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, huku wengine wakiacha vizuka na mayatima hakuna anaejali.

Amesema haiwezekani kuwa na ushindani wa kweli wa kisiasa, halafu Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume wanachaguliwa na Rais ambaye naye ni sehemu ya wagombea. Hali hii, alisema, inavunja misingi ya kidemokrasia na kuondoa matumaini ya wananchi kuona Zanzibar yenye siasa safi na uchaguzi wa haki.

Mgombea huyo alikumbusha historia ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), akibainisha kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwa nia njema na makubaliano ya wazi baina ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wa wakati huo.

Hata hivyo, amesema makubaliano hayo yalipuuzwa na kugeuzwa mtaji wa kisiasa bila kutekelezwa kikamilifu, jambo ambalo limeendelea kuidhalilisha Zanzibar.Alifafanua kuwa wananchi wa Zanzibar wamechoshwa na tume iliyogeuzwa kuwa chombo cha chama kimoja, na ndio maana ACT Wazalendo imeamua kwa mara kadhaa kudai mabadiliko makubwa, ikiwemo kuondoa utegemezi wa ZEC kwa Rais wa Zanzibar.

Othman ametoa mfano wa udhaifu wa tume hiyo kwa kueleza jinsi hata mpangilio wa karatasi za kupigia kura (Ballot Paper) unavyobeba CCM mbele ya macho ya wananchi.

Amesema ni jambo la aibu kuona chama kimoja kinapewa nafasi ya kwanza kwenye karatasi ya kura kila wakati, hali inayothibitisha upendeleo wa wazi na kuondoa imani ya wananchi katika chombo hicho.Aidha, alisisitiza kuwa serikali atakayoiongoza kupitia ACT Wazalendo itahakikisha tume mpya inaundwa kwa kuzingatia misingi ya uhuru, haki na uwakilishi wa kweli wa wananchi wote, ili kuepusha Zanzibar na mzunguko wa kisiasa unaoambatana na vurugu kila baada ya uchaguzi mkuu.

Amesema tume huru na yenye kuaminika ndiyo msingi wa uchaguzi wa haki, na bila kufanya hivyo Zanzibar itaendelea kuwa mateka wa migogoro ya kisiasa.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo ndiyo itakayojenga Zanzibar mpya yenye amani ya kudumu na maendeleo yanayomgusa kila mwananchi bila ubaguzi.

Kwa mara nyingine, Mgombea huyo alisisitiza kuwa Oktoba 29 ni siku ya maamuzi kwa kila Mzanzibari, kwani kupitia kura zao watakuwa na nafasi ya kuamua hatima ya nchi yao. Alisema kura ya mwaka huu siyo ya kawaida, bali ni kura ya ukombozi na kurejesha mamlaka ya wananchi juu ya mustakabali wa Zanzibar.

Huku hayo yakijiri mara baada ya hotuba hiyo, wazee mashuhuri wa Shehia ya Pujini walimpongeza Mgombea Urais huyo na kuahidi kumuunga mkono kwa dhati.

Mzee Suleiman Salim amesema wamefarijika kusikia dhamira ya ACT Wazalendo ya kuleta mageuzi ya kweli katika ZEC kwa kuwa chombo hicho kimekuwa kikwazo cha muda mrefu. “Sisi tumeshuhudia chaguzi nyingi, na tumekuwa tukiona matatizo yale yale kila wakati. Kauli ya Othman imetupa matumaini kuwa safari hii Zanzibar inaweza kuanza ukurasa mpya,” alisema.

Naye Mzee Khamis Ali amesema wananchi wamechoshwa na siasa za upendeleo na wizi wa kura, na sasa wanahitaji kiongozi mwenye ujasiri wa kusimamia haki. “Tunataka kuona kura ya kila Mzanzibari inahesabiwa na kuheshimiwa. Tunaamini Othman ana uwezo wa kutekeleza ahadi hii kwa vitendo,” amesema huku akishangiliwa na wenzake.

Kwa upande wake, Mwanakombo Hassan, mmoja wa wazee wa Pujini, amesema wanawake na vijana ndio wamekuwa wakipata mateso makubwa baada ya kila uchaguzi. “Tunataka mabadiliko, tunataka amani ya kudumu. Othman ametupa imani kuwa anaweza kulinda heshima ya kila mwananchi. Huu ndio wakati wetu wa kufanya maamuzi,” amesema kwa msisitizo.

Wazee hao wamehitimisha kwa kusema kuwa wako tayari kuhamasisha familia na jamii zao kuhakikisha kura zao Oktoba 29 zinampeleka madarakani Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, wakiamini kuwa ndiye kiongozi pekee mwenye dira ya kuibadilisha Zanzibar.