March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Urais ACT Wazalendo, aahidi kuirudisha hadhi ya Mji wa Chake Chake na kuinua uchumi wa Pemba

Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuurejeshea heshima na hadhi yake ya awali Mji wa Chake Chake, akisema Serikali yake italenga kuibadilisha Pemba kuwa kitovu cha biashara, maendeleo na ajira kwa vijana.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Chanjaani, Jimbo la Chake Chake, Othman amesema mji huo, ambao ulikuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi na kijamii, umedorora kutokana na sera zisizo sahihi na mfumo mbovu wa utawala wa sasa.

Amesema Chake Chake ilikuwa moyo wa uchumi wa Pemba, lakini leo imegeuzwa kuwa kijiji. Shughuli zote za biashara zimedumaa kutokana na mzigo mkubwa wa kodi na kukosekana kwa mipango madhubuti ya maendeleo.

Ameongeza kuwa mfumo duni wa Serikali uliopo umechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Pemba kuonekana kana kwamba ni eneo lililosahaulika na lenye maendeleo duni, huku miji yake ikipoteza mvuto wa kihistoria na kiuchumi.

Amesema chini ya utawala wa ACT Wazalendo, Serikali yake itaimarisha miundombinu ya miji yote, ikiwepo Chake Chake, Wete, Mkoani na Micheweni, kwa kuhakikisha huduma za kijamii, biashara na ajira zinapatikana kwa usawa.

Aidha, amesema Serikali yake itahakikisha hakuna Mzanzibari, hasa kutoka Pemba, atakayelazimika kuhama kwa sababu ya ugumu wa maisha, bali atapata mazingira rafiki ya kufanya shughuli zake na kustawi.

Othman amebainisha kuwa Pemba ina fursa kubwa za kimaendeleo ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kuinua uchumi wa wananchi. Alitaja sekta za uvuvi, utalii na kilimo kuwa msingi muhimu wa ustawi wa visiwa hivyo.

Amesema Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha Kisiwa cha Pemba kinakuwa eneo maalum la kiuchumi na kivutio cha watalii, huku wakazi wake wakinufaika moja kwa moja na miradi hiyo ya maendeleo.

Ameongeza kuwa katika Serikali yake, kodi zitaangaliwa upya ili kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, jambo litakalowasaidia kuongeza uzalishaji na kupanua masoko.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walimpongeza kwa sera zake zenye matumaini na maono makubwa kwa Zanzibar.

Mmoja wa wananchi, Asha Salim, amesema sera za mgombea huyo zimewapa matumaini makubwa hasa wanawake wafanyabiashara wadogo wanaokumbwa na changamoto ya kodi kubwa na ukosefu wa mitaji.

Naye Ali Khamis, kijana mkazi wa Chanjaani, amesema ahadi za Othman ni kielelezo cha kiongozi anayetambua changamoto za vijana na yuko tayari kuzitatua kwa vitendo, si maneno tu.

Wengine wamesema kuwa kwa mara ya kwanza wanamuona mgombea anayezungumzia masuala halisi yanayogusa maisha yao ya kila siku, kama uchumi, ajira na heshima ya miji ya Pemba.

Wamekubaliana kuwa kama sera hizo zitatekelezwa, basi Pemba itarejea kuwa kisiwa chenye maendeleo, ajira na matumaini kwa wananchi wote