March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Ubunge wa CCK ahidi mabadiliko Ilemela

*Ajikita katika kilimo,afya,elimu na ajira

*Kushirikiana na wataalamu kufanikisha vipaumbele vyake

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online – Mwanza

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Kijamii(CCK),Christina Blasio, ametaja vipaumbele vinne vya msingi atakavyovitekeleza endapo atachaguliwa kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Vipaumbele hivyo ni kilimo, afya, elimu na ajira, ambavyo amesema vinagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi.

Akizungumza na TimesMajira Online, Christina amesema dhamira yake ya kuwania Ubunge jimboni humo ni kuwa sauti ya wananchi wa Ilemela kwa  kuibua changamoto zinazowakabili ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu.

“Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa. Nikichaguliwa, nitahakikisha wakulima wa Ilemela wananufaika na elimu ya kilimo cha kisasa, hususani Cha umwagiliaji, ili kuongeza tija na kuondokana na kilimo cha mazoea,” amesema Christina.

Amesema kutokana na kukosekana kwa elimu ya kutosha juu ya kilimo bora cha umwagiliaji na matumizi ya mbegu bora kunachangia wakulima kupata mazao kidogo tofauti na matarajio.

“Nitaanzisha programu za mafunzo kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo ili kuwawezesha wananchi kufanya kilimo chenye tija  kwa ajili ya  chakula na biashara,”amesema Christina.

Katika sekta ya afya, Christina amesema atahakikisha wananchi wanapata elimu ya lishe bora kwa kushirikiana na wataalamu wa afya ili kupunguza magonjwa sugu kama kisukari, saratani na shinikizo la damu, yanayosababishwa kwa kiasi kikubwa na lishe duni.

Ameeleza pia kuwa ataweka mkazo katika afya ya akili kwa kushirikiana na wataalamu kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na hali ngumu ya maisha, hali inayosababisha migogoro katika familia nyingi.

Akizungumzia suala la ajira, Christina amesema ana mpango wa kuhakikisha vijana wanajengewa uwezo wa kujitegemea kupitia elimu  na kuweza kutumia  vipaji vyao kujiajiri na kuajiriwa.