Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara
MGOMBEA Ubunge kupitia chama Cha Sauti ya Umma (SAU) wa Jimbo la Musoma Mjini Christina Ndengo amewaomba Wananchi wa Jimbo hilo wamchague katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 ili akasaidie kupeleka msukumo kwa serikali ifufue viwanda vilivyosimama Vifanye kazi Kuwezesha utatuzi wa ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa Wananchi wa Musoma.
Amesema, kusimama kwa viwanda hivyo kumepelekea uchumi wa watu wa Musoma kushuka, huku Vijana wengi ambao wangepata ajira kwenye viwanda hivyo, kukosa suluhisho la tatizo hilo kutokana na baadhi yao kukosa mitaji ya kujiajiri.
Ameyasema hayo Septemba 14, 2025 wakati akizungumza katika ufunguzi wa Kampeni za chama hicho zilizofanyika katika maeneo ya Bweri Senta Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma. Ambapo pia amewanadi Wagombea wa Kata tatu wa nafasi ya udiwani waliogombea kupitia Chama hicho kati ya Kata 16 za Manispaa ya Musoma.
“Kusimama kwa viwanda kumepelekea wakulima wa pamba Kushindwa kulima pamba kwa wingi ndani ya Wilaya yetu, wakilima watauza wapi, kwa hiyo nikichaguliwa nitasimamia hili, pia hakuna maendeleo ya kilimo bila kuwa na viwanda ambavyo vinategemea malighafi kutoka shambani.”amesema Ndengo.

Kuhusuana na sekta ya elimu, mgombea huyo ameahidi kuwa kila shule ya sekondari katika Manispaa hiyo isiyokuwa na maabara itajengewa maabara ili kuwezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo ili wafaulu masomo hayo ambayo mchango wake ni mkubwa katika Mapinduzi ya viwanda.
Pia amesema, ataiomba serikali kuajiri walimu wa sayansi kwani uhaba wa walimu hao unaathiri kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi. Huku pia akiahidi kusimamia kwa uadilifu mfuko wa TASAF ili uwanufaishe walengwa ipasavyo.
Ametanabaisha pia ikipata ridhaa atahamasisha Vijana wa Musoma kuwa wabunifu wa kutumia teknolojia mbalimbali katika kujiletea maendeleo hasa kipindi hiki ambacho dunia imepiga hatua katika Mapinduzi ya viwanda.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Manispaa ya Musoma, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi, akisisitiza kuwa kura ndiyo silaha ya kuleta mabadiliko na kuchagua viongozi wanaofaa kuleta maendeleo katika jamii. Huku akiwaomba kuendelea kufanya kazi halali kwa bidii ili kujipatia kipato sambamba na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kwa namna yoyote ile.
Kwa upande wa huduma za afya, ndengo amesema atasimamia kwa nguvu sera ya matibabu bure kwa wazee wote, ambao wanatakiwa kupata matibabu kupitia utaratibu wa msamaha. amesema wazee wengi wamekuwa wakipata tabu kupata huduma bora, jambo ambalo analenga kulibadilisha ili waweze kuhudumiwa kwa heshima na kwa wakati.
Nao Wananchi waliohudhuria mkutano huo, wamesema watafurahi kuona Mbunge atakayeteuliwa anasimamia Kikamilifu utatuzi wa kero zao ikiwemo ujenzi wa barabara za pembezoni ambazo nyakati za mvua zimekuwa hazipitiki kwa urahisi.
“Barabara za Mtaa wa Nyabisare mvua zinaponyesha hazipitiki kirahisi ni vyema Mbunge ajaye aiombe serikali ikibidi itenge fedha zijengwe kwa kiwango cha lami.”amesema Juma Marwa Mkazi wa Bweri.
“Kata ya Bweri ni kubwa, tungepata Soko la Kisasa ingefaa sana, tungeuza biashara zetu kwa urahisi kama ambavyo Wananchi wa Kata ya Nyakato wanavyonufaika na soko ambalo lipo katika Kata yao Mbunge ajae aone hitaji hili ni muhimu .”amesema Joyce Petro.
Mgombea huyo , ameahidi kuwa sauti ya wanyonge ndani ya bunge endapo atapewa ridhaa ya kuwaongoza wakazi wa musoma mjini.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako