March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Ubunge kupitia CCK aahidi kuboresha miundombinu Ukerewe 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

 Mgombea Ubunge Jimbo la Ukerewe kupitia Chama Cha Kijamii(CCK),James Dioniz,ameahidi kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara pamoja na usafiri,jimboni humo endapo wananchi watampa ridhaa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.

 Akizungumza na Timesmajira Online, Dioniz amesema,amefanya maamuzi ya kugombea nafasi hiyo ili aweze kutatua changamoto mbalimbali zilizopo jimboni humo ikiwemo miundombinu katika sekta mbalimbali. 

Dioniz amesema,endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge katika Jimbo hilo, kipaumbele chake kikuu ni kushughulikia suala la miundombinu hasa ya barabara ambayo imekuwa ni changamoto kwa kuhakikisha inakuwa bora kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Ukerewe.

“Vivuko kwa ajili ya usafiri wa kwenda kwenye visiwa vingine jambo hili limekuwa tatizo sugu kwa miaka mingi, pia hatuna barabara nzuri za kupitia pamoja na huduma nyingine za usafirishaji,kwa mantiki hiyo nikiwa nimepewa ridhaa na wananchi wa Ukerewe nitashughulikia masuala hayo,”. 

Pia amesema,ili kurahisisha usafiri jimboni humo na kufanya kisiwa cha Ukerewe kufunguka kiuchumi na kuvutia wawekeza,akiwa Mbunge ataisukuma Serikali kukamilisha ujenzi wa daraja la vivuko cha Rugezi kwenda Kisorya.

 “Tutakapo fungua daraja hilo na kuunganisha na barabara za lami,litafungua fursa ya uwekezaji kwa sekta ya usafirishaji na vitu vingine.Huduma zitakuwa nzuri kwa sababu watu watakiwa na uhakika wa kutoka na kuingia ndani ya visiwa vyetu vya jimboni Ukerewe,”amesema Dioniz.

 Sanjari na hayo, Dioniz,amesema ataimarisha sekta ya utalii visiwani Ukerewe kwani kuna maeneo mengi ya kuvutia lakini hayajapewa kipaumbele. “Ukerewe ni visiwa ambavyo vimebarikiwa kuwa na fukwe nzuri ikiwemo Nansio,Ukara,Bweru,Ghana na maeneo mengine lakini havijapata wawekezaji na uwekezaji mzuri.

Kwa maana hiyo nitakapo kuwa Mbunge nitahakikisha tunazungumza na watu ambao wana uwezo wa kufanya uwekezaji katika fukwe zetu,ili kuinua sekta ya utalii katika eneo letu la visiwa vya Ukerewe,”amesema Dioniz.