Na Raphael Okello
Mara Mining Investment Ltd ni mgodi unaomilikiwa na mwekazaji Mzawa Josephat Mwita uliopo wilayani Tarime mkoani Mara.
Ambapo hivi Karibuni Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara ulitembelea mgodi huo chini ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mzee.
Kupitia ziara hiyo wananchi wa Kijiji cha Kerende wilayani Tarime wanaozunguka mgodi huo wanaanza kwa kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na mgodi.
Wanasema jambo la kwanza ni upandaji wa miti kuzunguka eneo hilo kwani hatua hiyo inawezesha kuwepo kwa utunzaji endeleavu wa mazingira .
Huku wakisema huo ni mwitikio wa maelekezo ya serikali katika kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa na kuepuka uharibifu wake ambao unasababisha athari kwa binadamu.
Miti zaidi ya 30,000 imeshapandwa na kazi ya kuhakikisha kuwa miti hiyo inatunzwa inaendelea.
Katika hatua hiyo kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara ilisisitiza kuwa upandaji wa miti katika maeneo ya migodi ni muhimu kufanywa na watu wote wanaojihusisha na uchimbaji wa madini .
Wananchi wa vijiji vya Karende, Mrito, Nyangoto, Gibaso na Kwihacha walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakisema kuwa hatua hiyo itafanya maeneo yao kuwa na hali ya ukijani .
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerende Muniko Mgabe anaushukuru mgodi huo kwa dhamira yake ya utunzaji wa mazingira pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo.
Mgabe anasisitiza kuwa suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa kila mgodi kutokana na shughuli wazifanyazo ambazo husababisha ardhi kuchimbwa umbali mrefu kwenda chini.
Pia anasema kutokana na changamoto ya uharibifu mazingira unaosababishwa na shughuli za wanadamu katika maeneo.
Mwenyekiti huyo anasema hapa duniani kunahitajika juhudi kubwa katika kunusuru hali hiyo na kwamba mwanadamu hana budi kufanya analoweza ili uwepo uendelevu wa sayari Dunia.
Anasema bioanuai ni muhimu kwa binadamu kwa namna nyingi ambapo mimea hutoa oksijeni na kusafisha hewa chafu .
Mgabe anafafanua kuwa mimea hutoa pia chakula, kivuli, vifaa vya ujenzi, dawa, nyuzi za nguo na karatasi huku mizizi ya mimea pia inapunguza mmomonyokowa udongo na kuzuia mafuriko.
“Mimea, fungi na wadudu hutunza rutuba na kusafisha maji kadri bioanuai inavyopungua husababisha mifumo hiyo kuharibika,”.
Anatoa mifano ya matumizi ya kemikali inayolenga kuangamiza wadudu wanao haribu mazao na kwamba dawa hizo zinaathiri wadudu wote.
Aidha katika nchi zenye matumizi makubwa ya dawa hizo ya kuua wadudu kwa ujumla imehatarisha ustawi wa mimea mingi pamoja na kilimo cha mazao.
Awali sekta ya madini ilikuwa ikimilikiwa na kudhibitiwa na serikali, sheria za uchimbaji madini ziligeuzwa katika miaka ya 1980 na 1990 na kuhusu umiliki binafsi wa migodi na kuingia kwa kampuni za kigeni.
Mwaka 2008 sekta ya madini iliajiri takribani watu milioni moja katika uchimbaji wa kienyeji.
Mwaka 2015 Benki ya Dunia iliipatia Tanzania mkopo wa takriban dola milioni 45 katika kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini.
Pamoja na hayo Mkurugezi wa Mara Mining Investment Josephat Mwita anasema licha ya mgodi huo kuwa na mikakati mizuri ya utunzaji wa mazingira pia umesaidia katika suala la vijana kupata ajira ambapo kwa sasa watu 300 wana ajira za kudumu na ajira za muda.
Vijana wengi walioajiriwa kwenye mgodi huo wanatoka vijiji vya Karende, Mrito, Nyangoto, Gibaso na Kwihacha.
Katika kufikia kuwa wachimbaji wa kati mgodi wa Mara Mining wanataka kuanza uchenjuaji dhahabu kwa teknolojia ya juu.
“Mgodi unakamilisha kulipa fidia wakazi hao ambao wapo maeneo ya mgodi huo ambapo mpaka sasa mgodi umeshalipa asimilia 85% kama fidia kwa wakazi waliokuwa kwenye eneo la mgodi na tunaendelea kulipa ili tukamilishe zoezi hilo,”anasema Mwita.
Anasema wao kama wachimbaji wazawa bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji ya kupanua kazi zao kwani benki hazikubali kuwakopesha.
Anataja changamoto nyingine ya watu wasio kuwa waamifu kuvamia eneo hilo kwa kujenga ili walipwe fidia na kuwepo kwa gharama kubwa za kukodi vifaa vya utafiti.
Sekta ya madini inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania hasa kwa uchimbaji wa shaba, dhahabu,fedha pamoja na baadhi ya madini ya viwandani na vito kama almasi.
Mwita anasema kuwa hatari inayowakabili wazawa ni kwamba kampuni za kimataifa za uchimbaji madini yanatawala sekta hiyo katika uchimbaji wa dhahabu na almasi, huku shughuli za ziada za uchimbaji mdogo zikitawanyika kote nchini na kufanywa na wachimbaji wadogo.
Anafafanua kuwa wachimbaji wadogo wanapaswa kuzingatia suala la mazingira na usalama.
Mwaka 2010 Tanzania ilikuwa ni nchi ya nne kwa kuzalisha dhahabu barani Afrika huku Tanzanite ikipatikana katika nchi hii pekee huku Afrika Kusini, Mali na Ghana zikifuata.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka anasema kuwa mgodi unapoanzishwa ni lazima ufanyiwe tathimini ya athari ya mazingira na mpango mkakati wa utunzaji wa mazingira kabla kuanzishwa.
Anasema hali hiyo inatakiwa kuendelea mgodi unapochimbwa na hatimaye unapofungwa ili kulinda mazingira nchini.
Anasema pamoja na migogoro ya kimazingira kati yake na jamii serikali uingia gharama kubwa ya kurekebisha mazingira yaliyoharibika.
“Hasara nyingine ya kutokuweka mpango mkakati wa namna ya ufungaji wa migodi pindi inapofungwa ni pamoja na kuacha mazingira katika hatari kwa afya ya jamii na viumbe wengine hai,”anasema Dkt.
Gwamaka.
Ni mkakati wa baraza hilo kuhakikisha historia mbaya ya utunzaji wa mazingira kwa migodi iliyoanzishwa kabla ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 hayatajitokeza tena kwenye migodi itakayoanza kuchimbwa kwenye awamu hii ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria kutoka NEMC Mhandisi Redempta Samwel amepongeza hatua zinazochukuliwa na miradi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa kuanzia hatua ya awali kabla ya shughuli za uchimbaji kuanza .
Anasema hatua hiyo ni nzuri katika kuweka usalama wa eneo la mgodi na maeneo yanayozunguka sehemu hiyo .
Mhandisi Redempta ameongeza kuwa baraza lina wajibu na mamlaka ya kisheria ya kufuatilia utekelezaji wa mpango mkakati ili kuepusha athari za kimazigira zinazoweza kujitokeza.
Meneja wa Kanda ya Ziwa Victoria NEMC Jerome Kayombo anasema wao wanataka migodi hapa nchini kuwa ni mfano kwa sababu kwa kufanya ushirikiano na wataalamu wa mazingira kuanzia hatua za mwanzo kabisa.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani