Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga.
SERIKALI imeshauriwa kuchukua hatua za makusudi ili kuweza kukabiliana na wimbi la vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kutokea katika maeneo mengi hapa nchini ikiwemo kundi la vijana wanaojiita “Panya Road.”
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ya wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mgeja amesema changamoto ya matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali yanayotokea hapa nchini hivi sasa inasababisha jamii kuishi na hofu muda wote kutokana na kutofahamu ni muda gani wahalifu hao watawavamia.
“Ukweli mimi nimepatwa na mshituko mkubwa kuhusiana na matukio haya ya uvamizi wa kundi la vijana wanaojiita “Panya Road” kutokana na jinsi wanavyopora mali za raia wema huku wakiwajeruhi kwa kutumia silaha mbalimbali na kuwasababishia wengine vilema vya maisha,”
“Binafsi naungana na watanzania wenzangu wapenda amani kulaani matukio haya yanayotokea, ambayo yanafanywa na vijana wetu wadogo kabisa, huu ni msiba mkubwa kwa Taifa, sasa lazima raia wema watoke na wasimame kutoa ushauri ili Serikali iyafanyie kazi ushauri wao,” anaeleza Mgeja.
Amesema hali hii inayojitokeza hivi sasa ni sawa watanzania kufuga “bomu” wao wenyewe na iwapo hali hiyo itaachwa iendelee huenda hapo baadae hali ikawa mbaya zaidi kuliko yanayoendelea hivi sasa na kwamba huenda yajayo yakawa mabaya zaidi kwa Taifa.
Amesema watoto hao wanaojiita kwa jina haramu maarufu “Panya road” ni matokeo ama zao la watoto wa Mitaani kwa jina ambao kwa kawaida wamezoeleka kuitwa “machokoraa” wanaozagaa kutwa mitaani na kulala maeneo hatarishi baadhi yao hufahamika kabisa wanatoka familia zipi na hawachukuliwi hatua zozote.
“Hawa atoto wa mitaani wanaoitwa chokoraa hivi sasa wamezagaa takriban kwenye mikoa yote hapa nchini na hasa maeneo ya Miji, Halmashauri za wilaya, Manispaa na Majiji na wanazidi kuongezeka siku hadi siku, sasa lazima tuchukue hatua mapema ya kukabiliana nao,” anaeleza Mgeja.
Mgeja amesema kuongezeka kwa makundi ya watoto wa mitaani (chokoraa) hapa nchini matokeo yake ndiyo sasa wamezalisha kundi jingine hatari ambalo ni hawa wanaojiita Panya road, na kwamba hali hiyo imechangiwa na wenye dhamana ya kuwaangalia kutochukua hatua mapema.
“Nafikiri ni wakati muafaka sasa kwa Serikali yetu kuanza kufanyia kazi tatizo hili la hawa Panya road, ukifanya uchunguzi utabaini lipo kundi kubwa sana, sasa endapo hakutakuwa na mkakati wowote au mpangilio mzuri na endelevu katika maeneo husika hawa watoto wa mitaani hapo baadae watakuwa hatari zaidi,” anaeleza.
Mgeja ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga amewaomba watanzania na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya Mitaa, Vitongoji, hadi Taifa wasingoje kila jambo mpaka Rais aseme hata mambo yanayohusu hao Panya Road na Chokoraa na kwamba Rais lazima asaidiwe na jamii yenyewe kwenye mambo ambayo wana uwezo nayo.
Mgeja ametoa ushauri wake kwa Serikali kwamba yapo mambo matano yanapaswa kufanyika katika kukabiliana na wimbi la Panya Road na watoto wa mitaani (chokoraa) kama itampendeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwemo kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi nchini.
Pia Halmashauri zote zitenge maeneo ya vituo vya kuwafunza kazi zenye ujuzi ambazo wanaweza kuzifanya kwa mikono yao na suala la maadili, kuwepo mkakati wa viongozi wa dini kuielimisha jamii jinsi ya kulea familia zao kimaadili hasa watoto sambamba na Halmashauri kutenga bajeti za ulinzi na usalama ili kusaidiana na Serikali Kuu.
“Lakini pia nafikiri ni wakati muafaka sasa pakaandaliwa kikao cha pamoja cha mawaziri watatu, Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, TAMISEMI na wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu ili waweke mkakati wa pamoja wa kushughulikia suala kuzagaa kwa watoto mitaani,” anaeleza Mgeja.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best