Na Moses Ng’wat,Timesmajira Online, Songwe
MGANGA Mfawidhi wa Zahanati ya Ipoloto Kata ya Bara wilayani Mbozi, Lyoba Nyamosi (34), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuiba dawa za binadamu mali ya serikali pamoja na vifaa tiba katika zahanati hiyo ya kijiji.
Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtumishi huyo alikamatwa Julai 19,2023 kwa ushirikianao kati ya jeshi hilo na wananchi.
Amesema mtumishi huyo alikamatwa baada ya kushitukiwa na wananchi akiwa na wenzake wawili ambao walifanikiwa kutoroka wakiwa na bodaboda mbili na baada ya kupekuliwa alikutwa akiwa ameficha dawa hizo kwenye mifuko ili zisionekane kirahisi.
“Mnamo Julai 19, 2023 majira ya saa 7:00 usiku mtuhumiwa alifika katika Zahanati hiyo akiwa na gari dogo kwa nia ya kuiba dawa na vifaa tiba, lakini kabla ya kubeba wananchi walimzingira na kufanikiwa kutoroka na gari,”amesema Kaimu Kamanda Ngonyani.
Ameongeza kuwa, baada mtuhumiwa kushindwa kutekeleza mpango wake wa kuiba dawa, alirudi kwa mara ya pili siku hiyo ya tukio majira ya saa 10:00 alfajiri akiwa na wenzake wawili kwenye bodaboda mbili.
“Kama haikutosha alifajiri majira ya saa 10:00 mtuhumiwa alirudi tena kwenye Zahanati hiyo akiwa na bodaboda mbili, kwa kuwa wananchi tayari waliweka mtego walifanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi lakini watu wengine waliokuwa kwenye bodaboda walifanikiwa kutoroka,” amefafanua Kaimu Kamanda Ngonyani.
Aidha, Kamanda Ngonyani amesema jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watu hao, pamoja na mtandao wa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakijihusisha na ununuzi wa dawa za serikali kinyume cha sheria.
Kaimu Kamanda Ngonyani ametaja dawa na vifaa tiba vilivyokamtwa kwa mtuhumiwa huyo kuwa ni vidonge vya uzazi wa mpango box 7 ambapo ndani yake kuna pakti 14, vidonge aina ya Cipro box 10.
Ametaja vifaa tiba vivyokamatwa kuwa ni bero 3 za vyandarua,bunda mbili za glovisi zinazotumika katika upasuaji, ikiwemo boksi 10 za glovisi aina ya Latex pamoja na dawa nyingine ambazo uchunguzi wake unaendelea.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM