April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo wa tehama unavyodhibiti utoro shuleni

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online

JAMII inatakiwa kwenda na mabadiliko ya Tehama katika shule mbalimbali nchini kwa lengo la kudhibiti utoro kwa wanafunzi na wazazi kufatilia matokeo ya watoto wao kwa urahisi Zaidi kwa njia ya kidigitali.

Mmoja wa waanzilishi wa Taasisi ya inayoshughulikia masuala ya elimu kwa njia ya Tehama(KILAKONA)ambaye pia ni Mkuu wa Operasheni kwa kampuni hiyo,Mohamed Mwinjuma amesema matumizi ya Tehama katika shule inasaidia kwa urahisi ufatiliaji wa mwanafunzi na kujua maendeleo yake.

Amesema kama nchi ni vema kwa sasa kuhakikisha inakua katika matumizi ya teknolojia na kufanya walimu kutumia mfumo huo kwa urahisi Zaidi katika uandaaji wa matokeo na uitishaji wa maudhurio kwa wanafunzi.

“Kupitia Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni muhimu kwa jamii kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwani historia ya siku ya mtoto wa afrika ilianzia huko afrika ya kusini kitongoji cha Soweto,Watoto waliandamana kwaajili ya kudai haki ya kupata elimu bora ambayo walikuwa wanapata Watoto wa kizungu tofauti na wao,”amesema

Mwijuma amesema Taasisi yao ya Kilakona inawasaidia watoto kupata elimu bora kwa miaka ya sasa kwani ni muhimu kwao kama wadau.

Baadhi ya viongozi wa taasisi ya inayoshughulikia masuala ya elimu kwa njia ya Tehama(KILAKONA) wakiwa katika picha ya pamoja.

kwa Upande wake Mkuu wa Utawala na Fedha Kampuni ya Kilakona na Kilakona Foundation, Jackline Mayalla amesema wamejipanga kujidhatiti kutengeneza kizazi ambacho kitakuwa na uwezo wa kutumia Tehama na kuonekana inawasaidia .

“Sisi kilakona tunajitahidi Tehama iwasaidie Watoto kwa njia ya maudhurio na katika ripoti za matokeo ya mtoto,njia ya tehama inamsaidia mzazi au mlezi kupata taarifa afikapo shuleni na anapoudhuria darasani kwa ujumbe mfupi wa simu yake,”amesema

Naye Meneja wa Data wa Taasisi hiyo,Tumainin Mwangonge amesema wao ni watetezi wa haki ya mtoto katika suala la elimu .

Amesema malengo yao ni kufikia Watoto laki tano katika awamu ya kwanza na wameanza kwa mikoa ya Pwani na kufikia shule nne za serikali na kutekeleza mfumo wa uhitaji majina kwa njia ya Tehama wanafunzi wanapokuwa darasani.

Mmoja wa Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Mtambani,Hamed Kondo amesema mfumo huo ni mzuri kwao kwani wazazi wanakuwa wanafatilia maendeleo ya Watoto wao moja kwa moja kupitia ujumbe mfupi wa simu.