December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo wa GePG waleta mageuzi makubwa ukusanyaji fedha za umma

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Arusha

KUANZISHWA kwa Mfumo wa Kielektoniki unaotumika kukusanya fedha zote za umma ujulikanao kama Government e-Payment Gateway (GePG) kumeleta mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa Arusha, Richard Kwitega, wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James chenye lengo la kuelimisha umma kuhusu mfumo wa kielektroni wa ukusanyaji wa fedha za umma jijini Arusha leo.

Akithibitisha jinsi mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa katika ukusanyaji fedha za umma, Kwitega amesema mwanzoni mwa mwaka wa Fedha 2020/21, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa kazi kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuufanyia thathmini ya kiutendaji Mfumo wa GePG.

Amesema Septemba, mwaka jana 2020, Taarifa ya tathmini ya kiutendaji ya Mfumo huu ilitolewa na wataalam wa Chuo cha Tehama cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoICT) ambapo ilibainika kuwa Mfumo wa GePG umewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ujumla wake na kwa taasisi moja moja.

Katibu Tawala wa Mkoa Arusha, Richard Kwitega, akifungua kikao kazi cha siku mbili cha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James chenye lengo la kuelimisha umma kuhusu mfumo wa kielektroni wa ukusanyaji wa fedha za umma ujulikanao kama Government e-Payment Gateway (GePG) ambao umeanza leo jijini Arusha. Kikao hicho kimeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Na mpiga picha wetu.

Ametoa mfano kuwa makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka sh. bilioni 95 kabla ya kuanza kwa mfumo hadi kufikia sh. bilioni 115 baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki.

Aidha, ametolea mfano Wakala wa Vipimo (WMA) akisema mapato yake yameongezeka kutoka kiasi cha sh. bilioni 1.0 kwa mwezi kabla ya Mfumo wa GePG hadi kiasi cha sh. bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG.

“Pia taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma,”amesema Kwitega.

Kwitega ametolea mfano Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) akisema ilikuwa ikilipa zaidi ya sh. bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme.

“Baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa shirika halilipi chochote,”amesema.

Ametafa faida nyingine za mfumo kwamba umewezesha kupatikana kwa taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo, kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa Fedha za Umma kwa taasisi zote za umma, kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa fedha za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji.

Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha-Wizara ya Fedha na Mipango, John Sausi, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kufungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Doto James..

Nyingine ni kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma, hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo, fedha kufika haraka katika Akaunti Kuu za Makusanyo zilizoko Benki Kuu, kusaidia benki na mitandao ya simu kuwa na sehemu moja tu ya kuunganisha mifumo yao na mifumo ya taasisi za umma, hivyo kuzifikia taasisi za umma na kutoa huduma za kifedha kwa urahisi.

“Mfumo umeziwezesha benki na mitandao ya Simu kuwa na mazingira rafiki na ya usawa katika ukusanyaji wa fedha za umma, kuzisaidia taasisi za umma kupunguza gharama zitokanazo na uwekezaji katika miundombinu ya Tehama pamoja na “Software Development” katika suala la ukusanyaji wa mapato,” amesema Kwitega.

Aidha, amesema mfumo huo urahisi katika usuluhishi wa miamala na usuluhishi wa taarifa za kibenki, kupunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji wa fedha za umma; kumuongezea mlipaji wa huduma za umma machaguo mengi ya njia za kulipia huduma za Umma (Benki za Biashara, Mawakala wa Benki na Mitandao ya simu yote sita na mawakala wanaotumia Mashine Maalum za Malipo zijulikanazo kama “Point of Sale – POS”.). Pia alisema mfumo huo umesaidia kuokoa muda.

Kwitega amesema Wizara ya Fedha na Mipango inatambua kuwa mafanikio ya mfumo huu wa GePG yanategemea sana ushiriki wa wananchi wote katika kuutumia.

“Hivyo, kila mwananchi anayelipia huduma yoyote ya umma ni lazima ahakikishe kuwa amepewa “Control number” na taasisi inayotoa huduma hiyo, na akiwa analipa ahakikishe amelipa kwa kutumia “Control number” hiyo,”alisema Kwitega.

Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimba vya habari wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao hicho, leo jijini Arusha.

Ametoa mwito kwa wahariri na wanahabari kutoa elimu kwa wananchi kutumia control number wanapofanya miamala ya Serikali, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na uhakika kwamba fedha walizolipa ziko salama na zimekwenda moja kwa moja mikononi mwa Serikali kwa ajili ya kuboresha maisha yao kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Serikali.

Ametoa mfano wa baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja la ule wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kutoa elimu bila ada kwa elimu ya msingi na sekondari, miradi ya kusambaza maji nchi nzima, kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na miradi mingine mingi ambayo utekelezaji wake unahitaji fedha nyingi.

“Kwa hiyo baada ya nyinyi kupata elimu hii, nanyi mtaifikisha kwa ukamilifu kwa umma wa Watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.

Iwapo umma wa watanzania utapatiwa elimu sahihi juu ya matumizi ya Mfumo wa GePG na kufahamishwa njia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia katika kufanya malipo ya Serikali katika namna rahisi na rafiki kupitia Mfumo wa GePG, itawezesha malipo mbalimbali ya Serikali kulipwa kwa wakatina kuongeza mapato yake,”amesema Kwitega.