November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo uondoshaji maji taka milimani wapongezwa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahya Rashid Abdulla, amepongeza juhudi za Serikali,kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),kubuni miradi ya usimamizi na uondoaji maji taka,katika maeneo yenye milima hususani katika Mkoa wa Mwanza.

Abdulla, ameeleza hayo Oktoba 8,2024,mara baada ya Kamati hiyo ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kutembelea mradi wa mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani ( Simplified Sewerage System),mtaa wa Pasiansi wilayani Ilemela ambao umenufaisha takribani nyumba 200 pamoja na mabwawa ya kutibu maji taka yaliopo Butuja,kutoka maeneo mbalimbali jijini Mwanza.

“Kwa kuwajengea miundombinu ambayo maji taka yanayotoka moja kwa moja nyumbani kwa wananchi,ni jambo jema,kwani awali yalikuwa yanaleta milipuko wa magonjwa kwa jamii.Sasa hivi yanatumika kama fursa,imesaidia kuondoa magonjwa ya milipuko na kuboresha mazingira ya wananchi kuishi katika maeneo yao,” amesema Abdulla na kuongeza.

“Kuna mambo tumejifunza na sisi kama Kamati tunayachukua,kwa sababu Serikali yetu inaelekea huko,ili kuboresha na kujenga mazingira mazuri katika eneo hili la maji taka, yaweze kutumika kama fursa ambayo tumeiona hapa Mwanza kupitia MWAUWASA,”.

Pia amesema,wanaamini kwa Zanzibar wakianza kutekeleza miradi kama huo,hautakuwa na gharama kubwa,kwani maeneo machache ndio yana milima ambayo mawe yake ni madogo.Tofauti na Mwanza ambayo ina milima ni mingi yenye mawe makubwa hali iliyochangia wananchi wake kupata shida katika kujenga hususani hata kuchimba choo.

“Zanzibar pia kuna maeneo ambayo wananchi wamejenga kiholela bila mpangilio,na kufuata ramani ya mpango miji na vijiji,hivyo kikubwa ndio hicho kilichotuleta Mwanza kujifunza,tumeona maboresho ambapo wananchi waliokuwa wanapata shida ya utitirishaji maji taka,sasa hivi wameondokana nayo,”.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar,Shaib Hassan Kaduara,amesema kila bahari mazingira yake yana stahili kutunzwa na kupata maji yanayoingia bila kuathiri viumbe maji waliopo ndani ya baharini.

Shaib,amesema utaalamu walioupata kutoka
MWAUWASA,wanaenda kusimamia kwani Zanzibar pia inapata changamoto kwa baadhi ya maeneo katika usamabazaji wa maji.

‘Sisi ambacho tumekiona huku kina changamoto,kwetu sisi inakuwa ni fursa ya kuweka sawa, na kile ambacho tumekiona kimefanikiwa tunaenda kuboresha zaidi,ili wote tujenge nchi yetu kwa pamoja”.

Hata hivyo amesema,Zanzibar ni Mji mkongwe, na tangu enzi hizo,mifereji ya utitirishaji maji taka ilikuwepo,ila imekuwa chakavu,hivyo kwa fursa ambayo wanaenda kuchukua baadae ya kusimamia,wataboresha mifereji hiyo ili iweze kutoa tija zaidi.

“Zanzibar maji ya bahati yanapanda na kushuka,
wakati maji yanatiririshwa kutoka nyumbani kwa wananchi,yanaingia baharini na kuondoka yakiwa hayajatibiwa.Hivyo sasa tunaenda kuyatibu ili yakiingia baharini viumbe hai visipate shida,”.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),Neli Msuya,amesema eneo la Butuja wana mabwawa 17, ya kutibu maji taka ambayo Yana uwezo wa kuchataka lita milioni 21 za maji hayo kwa siku.Huku kiasi wanachopeleka ni lita milioni 5 kwa siku.

“Maji taka yanapoingia katika bwawa la kwanza,yanatumia siku 6 hadi kufika katika bwawa la mwisho ambalo linaenda kumwaga maji ambayo yameishwa safishwa na kumwagwa kwenye Ziwa Victoria.Pia tunachukua vipimo sisi kama MWAUWASA, Bonde la Ziwa Victoria wanachukua vipimo pia,huku NEMC,wakitusimamia na matokeo ya vipimo ambavyo tunapewa yanaonesha maji taka haya yanasafishwa kwa ufanisi,”.

Pia ameeleza kuwa,wanachakata maji taka kutoa nyumbani kwa watu,na kuyaleta katika mabwawa hayo kwa njia tatu ikiwemo ya magari yanayokusanya maji taka maeneo ambayo hayana mfumo.

Huku njia nyingine ni mfumo maalumu wa kukusanya maji taka,kutoka kwenye nyumba zilizoko milimani, pia wana mabomba ya maji taka,ambayo yanakusanya maji taka katika maeneo ya katikati ya Jiji na kuyaleta kwenye mabwawa.

Sanjari na ameeleza kuwa changamoto ni maji ya mvua kuingia katika mfumo wa maji taka,hali inayowalazimu kutumia nguvu kubwa kuyakusanya na kuyamwaga kwani yanachangia uelemewe.Na wakati mwingine kusafisha mara kwa mara kutokana na maji ya mvua kuingiza mchanga katika mfumo huo.

Mwakilishi Jimbo la Mwanakwerekwe,Mjumbe wa Kamati hiyo,Ameir Abdallah Ameir,amesema wamejifunza tofauti za kijiografia lakini namna ambavyo MWAUWASA inavyowashirikisha wananchi katika miradi ya maji taka kwa asilimia kubwa.Hali ambayo inafanya wananchi wajione ni sehemu ya mradi na wanapaswa kwenda nao sambamba.