January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfuko wa SELF umetoa mikopo ya shilingi bilioni 313 kukuza uchumi wa Watanzania

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MFUKO wa SELF umesema toka kuanzishwa kwake  mwaka 2019 hadi Desemba mwaka 2022  umefanikiwa kutoa Mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 313 kwa wanufaika 225,000 nchini ili kukuza uchumi wa Watanzania.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 1,2023 na Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF Tawi la Dodoma ,Linda Mshana wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu Mfuko huo na shughuli zake katika kukuza uchumi wa Watanzania.

Mshana amesema kuwa lengo la mfuko huo ni kukuza na kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi hususan wa vijijini ili kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato ili kuondokana na umasikini.

“Sisi ni Taasisi ya huduma ndogo za fedha inayoongoza katika kubadili maisha ya watu hivyo mfuko unatoa huduma ya mikopo ya jumla(wholesale lending) na Mikopo kwa ajili ya mteja mmoja(retail lending )yenye masharti nafuu,”amesema Mshana.

Mshana ametaja aina za mikopo wanazozitoa kuwa ni Mkopo wa Kilimo,Mkopo wa Biashara,Mkopo wa Imarika,Mkopo wa Mtaji,Mkopo wa Mkulima,Mkopo wa Mshahara,Mkopo wa Pamoja na Mkopo wa Makazi.

Kwa upande wake Meneja wa Tawi la Dodoma,Aristide Tesha amefafanua kuwa Mfuko wa SELF ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha kwa wananchi wenye kipato cha chini ili kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato na kuondokana na umasiki.

Aidha amefafanua kuwa mfuko huo ulisajiliwa tarehe 14 Septemba 2014 chini ya Sheria ya kampuni ya mwaka 2002.

“Mfuko wa SELF ulianza kazi zake kama Kampuni Small Entrepreneurs Loan Facility(SELF)Project(1999/00 mpaka 2014/2015)na mwaka 2018 Serikali ilitoa uamuzi wa kuunganisha taasisi za UTT Microfinance Plc and SELF Microfinance Fund ili kukuza mtaji na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za mikopo kwa wananchi,”amesema Tesha.

Pamoja na hayo washiriki wa mafunzo hayo waliwatembelea maeneo ya biashara ya wanufaika wawili wa Mikopo hiyo ambao ni Aziza Nasib na Wema Sehaba.

Aziza Nasib ambaye ni mfanyabiashara wa kuchakata makopo ya maji yaliyotumika amesema kuwa amefanikiwa kukopa shilingi milioni 50 katika mfuko wa SELF ambao umemsaidia kuendeleza biashara yake na kupata mafanikio mbali mbali ikiwemo kununua magari ya biashara kwajili ya kusafirisha makopo hayo yanapochakwatwa kwenda kiwandani.

Naye Wema Sehaba wa WEMA AGROVET  ambaye anajishughilisha  na uuzaji pembejeo za kilimo amesema kuwa amefanikiwa kukopa milioni 40 katika mfuko wa SELF na zimemsaidia katika kukuza biashara yake ikiwemo kufungua matawi mengine ya biashara yake hadi vijijini.

“Mwanzo nilikuwa na duka moja lakini sasa hivi nina Duka lingine hapahapa mjini lakini nmefungua matawi vijijini kwasababu ya mkopo kutoka Mfuko wa SELF,”amesema Wema.