June 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meya Kumbilamoto akabidhi msaada unga wa sembe kwa mama lishe soko la nyama choma

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Dar

MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye ni  Diwani wa Kata ya Vingunguti,Omary Kumbilamoto,amekabidhi msaada wa unga wa sembe viroba 100 vyenye uzito wa kilo 5 kwa mama lishe na baba lishe 100 wanaofanya biashara Soko la Kisasa la Nyama choma la Kumbilamoto.

Kumbilamoto ametoa msaada huo jijini hapa leo Juni 2,2025 wenye jumla ya kilo 500 za unga, umetolewa na kampuni ya Azania Group kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara hao kuinuka kiuchumi baada ya kuhamia sokoni hapo hivi karibuni.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Kumbilamoto, ameishukuru Azania Group kwa kujitokeza kusaidia jamii, akieleza kuwa hatua hiyo ni ya kupongezwa na inaonesha mshikamano kati ya sekta binafsi na jamii.

“Nilienda kwa mmoja wa Wakurugenzi wa Azania Group na kueleza changamoto za wafanyabiashara hawa,bila kusita, walikubali ombi langu na kutoa unga huu. Niwapongeze sana kwa moyo wao wa huruma na mshikamano wa kweli,”amesema  Kumbilamoto.

Aidha, Meya Kumbilamoto aliwahimiza wafanyabiashara hao kuwaombea waliotoa msaada huo na kuendelea kuwa wavumilivu huku wakitumia msaada huo kama kichocheo cha kuimarisha biashara zao katika mazingira mapya ya soko hilo la kisasa.

Wafanyabiashara waliopokea msaada huo waliushukuru uongozi wa jiji na kampuni ya Azania Group kwa kuwaona na kuthamini mchango wao katika uchumi wa jiji, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa soko na halmashauri katika kuleta maendeleo.