November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meya wa Jiji la Mogadishu, Omar Mohamud Filish

Meya akosoa takwimu za vifo

MOGADISHU, Meya wa Jiji la Mogadishu, Omar Mohamud Filish amesema huenda virusi vya corona (Covid-19) vimeua watu zaidi ya 500 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita katika mji mkuu huo wa Somalia pekee.

Filish amekosoa takwimu za vifo na maambukizi ya Corona zinazotolewa na serikali akisisitiza kuwa haziakisi hali halisi katika nchi hiyo ya Pemba ya Afrika.

Alisema mji mkuu huo wa Somalia unarekodi kati ya vifo 19 na 49 vya Corona kila siku na kwamba, kuanzia Aprili 19, hadi Ijumaa ya mwishoni mwa wiki, jiji hilo lilikuwa limenakili zaidi ya vifo 500 vya wagonjwa wa Covid-19.

Wataalamu wa afya na wachimbaji makaburi nchini humo waliohojiwa na gazeti la The Gurdian la Uingereza walieleza wasiwasi kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaozikwa kila siku nchini Somalia.

Dereva mmoja wa gari la dharura kwa wagonjwa alisema, yeye binafsi huwa anabeba maiti 18 karibu kila siku kwa ajili ya kwenda kuzikwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kinyume na ilivyokuwa huko nyuma.

Waziri wa Afya wa Somalia, Fowziya Abikar Nur alitangaza kuwa nchi hiyo imerekodi kesi mpya 70 za Corona, na kupelekea idadi ya waliombukizwa virusi hivyo hadi sasa nchini humo kufikia 671.

Aidha, alisema watu watatu wamefariki kwa ugonjwa huo na kufanya idadi ya wahanga wa Corona mpaka sasa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kufikia 31, jambo linalopingwa.