Na Mwandishi wetu,Timesmajira,Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Bara, Christine Mndeme , amewataka viongozi wa Chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi viongozi wa serikali kufungua milango ya kusikiliza changamoto za wananchi na kutatua changamoto hizo kwa wakati.
Pia amewataka viongozi wa Chama hicho kutenga siku moja kusikiliza kero za wananchi na kuweza kuzitatua ipasavyo.
Akizungumza leo mkoani Dodoma wakati wa mapokezi ya Viongozi Wakuu wa Chama hicho,Mndeme amesema wanahitaji kuhakikisha Chama chao kinasimamia Serikali katika kushughulikia changamoto za wananchi na kuhakikisha kazi inaendelea na kutembea kifua mbele.
Amesema suala la viongozi mbalimbali wa Chama na serikali kufungua milango yao kusikiliza kero za wananchi ni jambo la muhimu kwao kwani lipo katika ilani ya Chama chao 2020/2025.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan anaumia sana kuona viongozi hawatatui kero za wananchi,huku kuna watu wanajifanya miungu watu,tunataka Chama kifungue mlango kipokee kero, kuzitatua na kusimamia kuziondoa kero kwa wananchi, “amesema na kuongeza
“Viongozi wasimamie wajibu wao katika Jumuiya mbalimbali za Chama iwe Vijana ,wazazi na wazee na kuhakikisha uhai wa Chama unaimarishwa kwa wanachama kulipa ada,”amesema
Aidha amesema ni jukumu la Chama kusimamia na kuhakikisha wanaisimamia serikali katika kuondoa urasimu katika maeneo mbalimbali na pia ni jukumu la Chama kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi halali ambazo ndio Msingi wa maendeleo.
“Tunakazi ya kufanya ndani ya Chama na Serikali lazima serikali tufanye kazi pamoja sisi kwa kushirikiana na Wabunge lazima tuhakikishe tunamsaidia Rais wetu,”amesema na kuongeza
“Rais wetu anayodhamira ya dhati kupeleka maendeleo ya nchi hii haraka kimaendeleo ,sisi sote lazma tumsaidie na tutimize wajibu wake na kama kuna mtu hawezi hatupishe,”amesema
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa