April 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchakato kugawanywa Jimbo la Mbeya Vijijini waiva

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imeanza mchakato wa kuligawa Jimbo la Mbeya Vijijini na kupata Jimbo jipya la Mbalizi katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Mchakato huo wa kugawanywa kwa  Jimbo la Mbeya Vijijini limeafikiwa Machi 12,2025 na wajumbe wa baraza la ushauri wilaya ya Mbeya (DCC),kutokana na ukubwa wa jiografia wa jimbo hilo ulivyo.

Akitoa mapendekezo ya kamati ya wataalam na madiwani, Ofisa utumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya ambaye pia ni mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi,Daudi Mbembela amesema kusudi na pendekezo lililopo ni kugawa jimbo hilo kuwa na majimbo mawili ya Mbalizi litakalounganisha Tarafa ya Isangati na Usongwe na jimbo la Mbeya litakalotokana na tarafa ya Tembela.

“Kusudio la kugawa  Jimbo hili ni kutokana na ukubwa wake ulivyo ndo sababu ya kuwepo kwa mapendekezo ya kuligawa Jimbo hili Kutokana na wananchi kukabiliwa na changamoto mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini ,Akimu Mwalupindi, amesema jimbo hilo ni kubwa hivyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utendaji kazi hivyo kuendelea kuwaasa watumishi, viongozi wa kisiasa kuhakikisha maeneo yao yanalindwa kwa kutopokwa kwenda kwenye maeneo mengine ya kiutawala.

Mwenyekiti wa kikao hicho,Mkuu wa wilaya ya Rungwe Jaffary Haniu kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Mbeya Beno Malisa, ambaye amesisitiza umoja na mshkamano kwa watumishi na wananchi wilayani Mbeya kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia wananchi na kuhimiza ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya hiyo.

Pia amesema maoni yaliyotolewa kwenye kikao hicho yamechukuliwa ili kwenda kuwasilishwa kwenye kikao cha ushauri mkoa RCC ili nao waweze kuwasilisha ngazi za juu  huku akiwataka wana Mbeya vijijini kuendelea kuwa watulivu.