January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchakato kufufua Shirika la TAFICO wazidi kushika kasi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

MCHAKATO wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) unazidi kushika kasi lengo likiwa ni kuiwezesha nchi kuzifikia na kunufaika na rasilimali za uvuvi, hususani zilizopo katika ukanda wa uchumi wa bahari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO, Esther Mulyila, amesema Serikali iliona kufufua shirika hilo kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi ili iweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Kupitia TAFICO, nchi itaweza kuzifikia, kuzitumia na kunufaika na rasilimali zake za uvuvi hususan zilizopo katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu ( Exclusive Economic Zone-EEZ) ili kukidhi mahitaji ya nchi ya sasa ya kufikia uchumi wa viwanda,” amesema Mulyila.

Kwa mujibu wa Mulyila tangu uhuru nchi yetu haijanufaika kikamilifu na rasilimali za uvuvi, bali imekuwa ikinufaika kwa kuzipa leseni zinazotolewa kwa meli za kigeni kwa ajili ya kufanya uvuvi na tozo mbalimbali.

Alisema hatua ya kwanza ya kufufua shirika hilo, itawezesha nchi kunufaika na rasilimali hizo ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.

Akieleza mchakato wa kufufua TAFICO ulivyoanza, Mulyila amesema Serikali ilianza kwa kuunda timu ya kukimbiza kazi za kiutawala na kwamba tayari wamemaliza kuandika taarifa ya muundo wa shirika hilo litakavyokuwa.

“Pia hatua nyingine ilikuwa ni kutafuta vyanzo vya fedha na kuishauri Serikali,” alisema Mulyila. Hata hivyo alisema katika eneo hilo walikutana na changamoto ya watu kutotaka kuwekeza kwenye Uvuvi wa Bahari Kuu kwa sababu ya ugumu na mtaji unaohitajika kuwa mkubwa.

“Kwa hiyo ilibidi sasa tuanze kutafuta vyanzo vya fedha na hili tumeendelea nalo. Upatikanaji wa vyanzo vya fedha ulikuwa mgumu hata kupata wabia. Kumbuka maelekezo yalikuwa ni kufufua shirika kwa ubia,” alisema Mulyila na kuongeza;

“Tulianza kutengeneza mpango wa biashara ambao tayari umetengenezwa.”

Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO, Esther Mulyila, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuhusiana na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukulia kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO). Na mpiga picha wetu.

Alifafanua kwamba kwenye mpango huo wa biashara unaainisha miradi 10 itakayoendeshwa na TAFICO katika kipindi cha miaka 10 ya kwanza.

Kwa mujibu wa meneja huyo, miradi hiyo 10 imegawanyika katika maeneo makubwa matatu ambayo yanapanua muundo wa TAFICO ya sasa.

Mulyila amesema eneo la kwanza linahusu miradi ya uvuvi, ambao ni kununua meli na kuziendesha. “Kwa hiyo mradi wa kwanza ni kununua meli ya uvuvi.

Amefafanua kwamba meli hiyo ikianza kufanya biashara wanataka iwe ni mradi unaojitegemea na itakuwa ikijiendesha kibiashara.

Pia, amesema wanataka kuwa na meli ya uvuvi itakayokuwa inakwenda kuvua samaki kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu kwa kutumia uvuvi aina ya mishipi.

“Ndiyo maana tunataka hiyo meli tuhakikishe inajiendesha kibiashara, kama inasababisha hasara, basi tujue tunapata hasara wapi,” amesema Mulyila na kuongeza;

“Meli ya kwanza itakuwa ni ya uvuvi wa kutumia mishipi na hii ndiyo meli ya kwanza inayokuja tunaitegemea Juni, mwakani, kwani tayari mchakato wa kuiunda umeanza na itakuwa na urefu wa mita 22.”

Alisema meli hiyo ina nguvu ya kukaa Bahari Kuu siku 30 kama haijajaza mzigo. Amesema meli hiyo itakuwa na injini kubwa na vifaa vya kisasa.

“Kwa hiyo meli hii ya kwanza itakuwa ni ya uvuvi wa mishipi yenye urefu wa kilometa 23 hadi 25 unaotumia ndoano,” amesema na kuongeza kwamba mshipi mmoja utakuwa na ndoano 500.

Akieleza sababu ya uvuvi wa kutumia mishipi, meneja huyo alisema samaki aina ya jodari wa kiwango cha juu wanaotakiwa sana kwenye soko ni wa uvuvi wa kutumia mishipi.

Kwenye ndoano hizo alisema chambo itakuwa ni samaki aina ya ngisi au vibua, hivyo wavuvi wetu hapa nchini watakuwa wamepata soko la kuuza samaki wao kwa TAFICO

***Wazo la kufufua TAFICO

Akizungumzia chimbuko la kufufuliwa kwa TAFICO, meneja huyo amesema hayo ni matokeo ya maono ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Amesema baada ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kuingia madarakani iliongeza nguvu na kasi ya kufufua TAFICO

Amesema hata Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ambayo inaishia mwaka huu, Rais Magufuli aliahidi kununua meli tano za uvuvi wa Bahari Kuu.

“Kwa hiyo suala ilikuwa ni meli hizo zitafanyaje kazi wakati Serikali haifanyi biashara? Ndipo Serikali iliona umuhimu wa kuanzisha chombo cha Serikali kitakachosimamia uratibu wa shughuli za uvuvi wa kibiashara na ndipo ikaonekana sasa kufufuliwe TAFICO ili iwe ni mkono wa Serikali katika shughuli za kibiashara katika shughuli za uvuvi,” amesema

Kwa mujibu wa meneja huyo baada ya Serikali kutangaza kufufua Shirika hilo, jitihada za kufufua shirika zilikuwa chini kwa sababu ya kuwepo kwa kesi mahakamani.

Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani Februali 2015 na kwamba mwaka 2018 ndipo kesi iliisha na utekelezaji wa maelekezo ya kufufua shirika yalianza.

TAFICO ni shirika la umma chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambalo linamiliki mali zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 118 kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi mwaka 2017.