December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Regina Ndege, kuacha alama ya kihistoria ifikapo 2025

Na Mary Margwe, TimesMajira Online, Babati

Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Manyara Regina Ndege amesema ataacha alama ya kihistoria ifikapo 2025 Mkoani humo,ambapo ametoa mifuko 100 ya saruji na matofali 200 kwaajili ya kuchangia mradi wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT unaendelea katika Wilaya za Mkoa huo.

Hayo alibainisha hivi karibuni wakati alipokua akizungumza kwenye kikao Cha baraza la UWT Mkoani humo, ambapo alisema kila Wilaya sasa inaendelea na kutafuta miraji pamoja na ujenzi wa nyumba hizo za watumishi wa UWT pamoja na miradi mingine itakayowainua kiuchumi.

Ndege alisema ni lazima aache alama ifikapo 2025 Kwa Umoja wa Wanawake wa Tanzania ( UWT ) Mkoani Manyara, amesema anawashukuru wakina mama wa mkoa huo kwa kumfikisha hapo alipo, kwa kile alichodai kuwa bila ya wao asingefika hapo alipo hivyo hatowaacha bila kuwaachia alama katika Wilaya husika kama kumbukumbu yake kwao.

” Alama nitakayoiacha nitahakikisha nachangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi unaoendelea sasa wa nyumba za Makatibu UWT pamoja na ujenzi wa miradi mingine ili majengo yasimame, ambapo tayari nimetoa mifuko 100 ya saruji kwa Wilaya ya Kiteto, matofali 500 kati ya 1000 nimekabidhi juzi kwa uongozi wa UWT Mji wa Babati chini ya Mwenyekiti wetu Eva Luoga na katibu wa UWT Zainabu Dodo, na pia matofali 500 kati ya 1000 nimekabidhi Wilaya ya Babati kwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo Aghata Tsere, na Katibu wakewa UWT Wilaya hiyo Tupilike Kabejela” alisema Mbunge huyo

” Wakati nilipofanya ziara ya kwanza nilihamasisha kila Wilaya kuanzisha miradi, jambo ambalo nililifanya Kwa Wilaya zote 5 za Mkoa huu, Nilipofanya ziara ya pili nilihamasisha kwa kuendelea kwa kuahidi lakini nashukuru nimeanza kutekeleza ahadi zangu” aliongeza Regina Ndege.

Aidha mbali na kutoa mifuko 100 ya Saruji kwa Wilaya ya Kiteto, pia ametoa mafofali 500 kati ya 1000 aliyoahidi Babati Mjini chini ya Mwenyekiti wake wa UWT Eva Luoga, Katibu wake Zainabu Dodo, Wilaya ya Babati pia aliahidi matofali 1000 tayari ametoa 500, wakati wa ziara yake aliyoifanya Oktoba Mwaka Jana.

” Lakini Wilaya ya Simanjiro, Mbulu, na Wilaya Hanang, wote wanataka kuanza ujenzi, na wananisumbua kweli kweli kwamba tekelezwa ahadi, Mimi nakwenda kwa awamu japo siwezi kutoa mara moja kwa Wilaya zote, kwahiyo kila Wilaya nina uhakika mpaka mwezi Machi nitakua nimeanza kukamilisha zile ahadi zangu, nikuhakikishie hilo Mh.Mwenyekiti” aliongeza Ndege.

Alisema kutoa mifuko 100 ya saruji na matofali 200 Kwa hizo Wilaya mbili haiamanishi ataishia hapo, ujenzi utaendelea na kwakua ujenzi unaendelea hatakwamia hapo atahakikisha ataendelea kuchangia hadi pale ujenzi huo utakapokamilika, hivyo kila Wilaya itambue hilo kikubwa ni kuombeana uhai na maisha yenye afya.

Aidha alisema katika uongozi wake ifikapo 2025 atahakikisha kila Wilaya itakua na mradi kama walivyokubaliana lakini nyumba za watumishi, zitakapojengwa miradi kwenye Wilaya hizo, Mkoa hawatauacha, ambapo pia aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji, ambapo amesema kwenye Uongozi wake atahakikisha anaacha alama katika Mkoa huo hususani katika nyumba za makatibu wa UWT Wilaya pamoja na miradi mingine

Mbali ya hilo aliwataka Wajumbe hao na viongozi mbalimbali kwanujumla kuhakikisha wanaendelea kushikamana, kuendelea kudumisha umoja wao, lakini waendelee kuchapa kazi kikamilifu, ili kuweza kutimiza ahadi zao na hatimaye kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa UWT Mkoani hapo Fatuma Tsea alimtaka Mbunge Regina Ndege kutokufanya ziara zake kimya kimya na badala yake amemtaka kuwashirikisha viongozi mbalimbali.

MMbunge wa Viti Maalum Mkoani Manyara Regina Ndege akikagua nyumba ya Mtumishi wa UWT Mji wa Babati, ujenzi unaendelea katika Kata ya Baghara kwa moto, mara baada ya kukabidhi matofali 500 kati ya 1000 aliyoahidi, Picha na Mary Margwe.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Manyara Regina Ndege kulia, akikabidhi matofari Kwa Katibu wa UWT Mji wa Babati Zainabu Dodo, Kwa ajili ya ujenzi unaendelea ya nyumba ya Mtumishi wa UWT Mji wa Babati katika Kata ya Baghara kwa moto, Picha na Mary Margwe.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Manyara Mh. Regina Ndege wa pili kulia, akikabidhi moja ya matofali 500 kati ya 1000 aliyoahidi kwa uongozi wa UWT Mji wa Babati Kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT Mji wa Babati, ujenzi unaendelea katika Kata ya Baghara kwa moto, Picha na Mary Margwe