Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,ametoa kiasi cha milioni 4,kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji kwa mtaa wa Kangaye Kata ya Nyakato.
Fedha hizo ambazo zimetolewa kutoka katika mfuko wa Jimbo,ili kuweza kusaidia mtaa huo kupata maji na kutatua changamoto inayowakabili kwa sasa.
Dkt.Angeline amechangia kiasi hicho kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kangaye Kata ya Nyakato,wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero, changamoto, ushauri na pongezi kutoka kwa wananchi,mkutano uliofanyika uwanja wa Kangaye Center,jimboni Ilemela mkoani Mwanza.
Dkt.Angeline ameeleza kuwa pamoja na nguvu za serikali lakini wananchi wamechangia pia nguvu zao hivyo ameunga mkono juhudi hizo.
Ambapo wananchi wamechangishana kiasi cha milioni moja kwa ajili ya kumaliza kero ya maji hivyo na yeye kupitia mfuko wa Jimbo amechangia kiasi hicho cha fedha ili kuhakikisha kero hiyo inatatuliwa.
Ameeleza kuwa mbali na hayo pia wananchi hao waneendekea kuchochea utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo yao ambapo mbali na sekta ya maji pia wamegusa sekta ya elimu kwa kuchangia ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Kangaye.
Pia Mbunge huyo katika kuendelea kuwaunga mkono wananchi katika sekta ya elimu amechangia kiasi cha laki nne(400,000), kwa ajili ya kuweka umeme katika shule ya msingi Kangaye.
Awali mmoja wa wananchi wa mtaa wa Kangaye Agnes Mafuta,alimuomba Mbunge huyo kuzipatia ufumbuzi changamoto ya ukosefu wa huduma za maji safi na salama, ubovu wa barabara pamoja na kukatika katika kwa nishati ya umeme.
Akitolea ufafanuzi changamoto ya ukosefu wa huduma ya uhakika wa maji Mhandisi wa Idara ya maji safi na maji taka wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la jijini Mwanza (MWAUWASA) Fute David,mamlaka inaendelea na juhudi za kutatua kero hiyo ambapo sasa inaendelea na utekelezaji wa mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba.
Amefafanya kuwa kutokana na uzalishaji mdogo ambao hauendani na mahitaji halisi ya maji,wanafanya mgao wa huduma za maji ili kila mwananchi apate pamoja na kuchimba visima vitakavyorahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Hivyo amewaomba wananchi hao kuwa wavumilivu kwani mamlaka hiyo inaendelea na jitihada za kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Diwani wa Kata ya Nyakato Jonathan Mkumba,ameahidi kuwa kusimamia fedha zilizotolewa hili zitumike kwa malengo mahususi yaliyokusudiwa huku akimshukuru Mbunge huyo kwa kuwaunga mkono.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mhandisi Modest Apolinary,amewahimiza wananchi wote wenye changamoto za upimaji wa ardhi kuandika malalamiko yao katika ofisi za watendaji wa kata zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Huku akieleza kuwa zaidi ya milioni 550 imetolewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kipindi cha miezi sita.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua