December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, Rhoda Kunchela.

Mbunge CHADEMA asema ni wajibu wao kukichangia chama

Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma

Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rhoda Kunchela amesema, yeye kama Mbunge ni wajibu wake kukichangia chama, kwani chama kinatumia fedha kwa ajili ya kujiendesha.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye mahojiano ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma.

Amesema,michango ya chama ipo kikatiba na kuchangia ni lazima na siyo ombi wala hiyari, kwani fedha zilizolalamikiwa na wabunge zinafanya kazi nzuri ya kuimarisha chama.

Kunchela amesema,matumizi ya fedha hizo yanaonekana kwa vitu mbalimbali vinavyonunuliwa na operesheni za chama zinazofanyika nchini kote.

“Nimehojiwa nimeyajibu yale ambayo ninayafahamu, kwa sababu nimeona masuala ya fedha mengi sana yalikuwa hiyari yangu, kwa sababu nimekuwa nikiona shughuli za chama, chama kinatumia fedha, kwa hiyo kwangu mahojiano yalikuwa sawasawa na chama kipo sahihi, kwa sababu ukiangalia CAG katika ripoti yake amesema kwamba chama chetu kimepata hatia safi baada ya kufanya mahesabu yote, kwa hiyo michango ya kichama hiyo milioni moja na laki tano ni ya kikatiba na lazima tuchange na si ombi, ni lazima uchange, na si ombi, na kabla ya kuwa Mbunge nilikuwa nafahamu umuhimu huo wa kukichangia chama na tutaendelea kuchanga,”amesema Mbunge huyo.