November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge atoa mil 3 kuboresha sekta ya michezo,sanaa Nsimbo

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Nsimbo.

Zaidi ya milioni 3.5 zimetolewa kwa vikundi mbalimbali vya michezo na sanaa katika Kijiji cha Mtakumbuka Kata ya Kapalala Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoa wa Katavi kwa ajili ya kuinua michezo na sanaa mkoani humo.

Akitoa fedha hizo leo Julai 28,2023 Mbunge wa Jimbo la Nsimbo,Anna Lupembe ameeleza kuwa ni msimu wa tatu amekuwa akifadhili mashindano mbalimbali ya michezo hususani mpira wa miguu kupitia ligi ya Lupembe Cup ambayo lengo ni kuibua vipaji kwa vijana huku akitambua michezo sio kwa ajili ya kujenga afya pekee bali ni ajira.

Lupembe amesema kwa msimu wa mwaka 2023 amedhamiria kuibua vipaji vya sanaa kwa vijana husasani vya ngoma asili,muziki wa kizazi kipya na kwaya kwa njia ya kufanya bonaza kwa kila Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo.Mbunge huyo amesema kuwa bonaza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inawataka kukuza michezo na kuibua vipaji.

Ameweka wazi kuwa michezo na sanaa kama vijana watazingatia kufanya kwa bidii watakuwa sehemu ya kushiriki kwenye kukuza uchumi wa nchi huku na uchumi wao ukiimarika.

Bonaza hilo limeshindanisha vikundi mbalimbali vya sanaa na washindi kupatikana ambapo Mshindi wa kwanza amepata 300,000 huku washindi wawili wa nafasi ya pili kila mmoja amepatiwa kiasi cha 200,000.

Hata hivyo washindi wa saba wa nafasi ya tatu kila mmoja amejipatia kiasi cha 100,000, washindi sita wa nafasi ya nne kila mmoja 50,000,washindi nane wa nafasi ya tano kila mmoja 25,000 ,washindi wawili wa nafasi ya sita kila mmoja 20,000 walioshika nafasi ya saba ambao walikuwa wawili kila mmoja alihipatia 10,000 kama kifuta jasho.

Washindi wa ligi ya Lupembe Cup kwa ngazi ya Kata ya Kapalala mshindi wa kwanza amepewa kiasi cha 500,000,mshindi wa pili 300,000, huku mshindi wa tatu 100,000 na mshidi wa nne 50,000.

Lupembe amesema kuwa kwa mshindi wa nafasi ya kwanza na ya pili kwenye sanaa watashiriki moja kwa moja kwenye bonaza ngazi ya Jimbo ambapo mshindi atakaye patikana atapewa kiasi cha 1,000,000 sambamba na kuchukuliwa kwenda kwenye mashindano ya sanaa Jijini Mbeya yanayoratibiwa na Spika wa Bunge,Dkt.Tulia Ackson.

Aidha katika mashindano ya ngazi ya Jimbo yatatumika kwa ajili ya kuchangua vijana 40,wenye vipaji maalumu ili kupelekwa kambi kama sehemu ya mchakato wa kutengeneza timu ya Nsimbo ambapo itakuwa sehemu ya kuanza kushiriki mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu kuelekea Ligi Kuu Tanzania Bara-NBC.