April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge ataka safari za ndege kuanzia Dodoma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MBUNGE wa Ilemela Dkt.Angelina Mabula amehoji Mpango wa Serikali wa kuanza kwa safari za anga Kutoka Dodoma-Mwanza,Dodoma-Mbeya na Dodoma-Arusha Ili kupunguza gharama kwa wasafiri wanaokwebda Mikoa hiyo.

“Je, lini ATCL itaanzisha usafiri wa Ndege kutoka Dodoma – Mwanza – Mbeya na Arusha ili kupunguza gharama kwa Wasafiri wanaokwenda Mikoa hiyo.”amehoji Dkt.Mabula

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo Aprili 15,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi Cha maswali huku akiitaka Serikali kutoa jibu la uhakika ni lini safari hizo zitaanza kwani ameshauliza awali hilo mara tatu na majibu yamekuwa ni ya kutia faraja kwamba safari zitaanza lakini hakuna kinachofanyika.

Akijibu swali hilo,Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema,
Safari za Dodoma – Mwanza zinatarajiwa kuanza Desemba 2025, huku tathmini ikiendelea kwa safari za Dodoma – Mbeya na Dodoma – Arusha.

Dkt.Mabula amesema,ikumbukwe uwanja wa Ndege wa Mwanza ni lango la Miji ya Maziwa Makuu lakini pia Mwanza ni mji wa pili kwa ukuaji wa uchumi na abiria wengi wanatoka Kanda ya ziwa,lakini pia Makao Makuu sasa ni Dodoma huku akisema kuwepo kwa safari hizo kutaondoa usumbufu wa watu kusafiri Mwanza Hadi Dar es Salaam ndipo warudi Dodoma.

Kihenzile , amesema Shirika la ndege la ATCL linaendelea kupanua mtandao wa safari kwa kuzingatia mpango mkakati wake na mahitaji ya soko. Kwa sasa, ATCL inahudumia vituo 26 kutokea Dar es Salaam vikiwemo vituo 14 vya ndani ya nchi.

Vile vile Dkt.Mabula amehoji kama Serikali haioni kuwa ni muda muafaka wa kuzungumza na mashirika Binafsi ya ndege Ili waweze kuwa na ndege kubwa na kufanya kazi ya kuongeza safari hizo za Mwanza-Dodoma,Dodoma-Arusha na Dodoma- Mbeya Ili kukuza uchumi wa Taifa kwa usafiri wa anga.

Akijibu Kihenzile amesema,
Serikali imefanya jitihada kubwa za kuboresha usafiri nchini ukiwemo wa anga huku akitolea mfano wa miaka Tisa nyuma iliyopita Taifa lilikuwa na ndege Moja tu lakini sasa Serikali imenunua ndege 16 ikiwemo ndege ya mizigo .

Hata hivyo amesema ,mahitaji ni makubwa na hivi sasa Serikali inaboresha viwanja vya ndege karibu Nchi mzima ambavyo havijakamilika.

“Vitakapokamilika,wabunge wa maeneo hayo pia nao watakuwa wakisimama Bungeni kuhitaji ndege.”amesema Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo nichukue ushauri wake wa pili na ninayaagiza mashirika Binafsi ya ndege ndani na nje ya Nchi watazame fursa ambayo Serikali imewekeza ya kujenga viwanja vya ndege karibu kila mkoa waone namna gani wataboresha usafiri lakini na wao watafanya biashara”