November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge aomba sh.2.5 bil kurejesha miundombinu ya barabara

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MBUNGE wa jimbo la Kishapu Boniface Butondo (CCM)  ameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) iwasaidie kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kurudisha hali ya miundombinu ya barabara katika wilaya ya Kishapu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.

Akizungumza leo April 8,2024 wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Butondo amesema kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini zinasababisha uharibifu mkubwa wa barabara katika maeneo mengi.

Amesema moja ya maeneo yaliyoathiriwa ni pamoja na wilaya ya Kisahapu ambapo kuna uharibifu mkubwa wa barabara,Makaravati  ,madaraja na hata barabara kuzolewa kabisa .

“Hivi ninavyozungumza tathimini ya muda mfupi iliyofanyika ,ni zaidi ya kilomita 53 za barabara  zimeharibiwa kabisa katika kata mbalimbali za Kishapu,kwa hiyo tunaiomba TARURA itusaidie angalau shilingi bilioni  2.5 ili zitusaidie kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibiwa kwa sababu zaidi ya kata sita hazina mawasiliano kabisa.”amesema Butondo
 Aidha ameishauri  Serikali ifanye jitihada za kuhakikisha inarudishia miundombinu hiyo ili jitihada za Kimaendeleo ziweze kuendelea vizuri
Vile vie amezungumzia barabara ya Kishapu ambayo inatoka Kolandoto -Kishapu -Mwangongwa wilaya ya Maswa  yenye mrefu wa kilomita 65,ameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ijenge barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani imeshakuwa katia mpango wa bajeti wa muda mrefu.

“Barabara  hii kwa kipindi kirefu imekuwa ikipangwa katika mpango wa bajeti kwa takriban zaidi ya miaka 7 au 8 lakini haijengwi,kitu hiki hakipendezi,lakini pia kwenye
Ilani ya Cgama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015/2020 ilikuwepo lakini haikutekelezwa na leo tunakwenda mwaka wa nne kipindi cha 2020/2025 haijatekelezwa, japokuwa imo kwenye mpango wa bajeti lakini hili ili halileti afya hata kidogo,

“Licha ya Serikali kufanya mambo makubwa lakini katika eneo hili wanakishapu bado tunakwazwa,ni  wajibu wa Serikali yetu kuhakikisha inatekeleza ujenzi wa barabara hii katika kiwango cha lami.”amesisitiza Butondo