February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge aja na uvuvi wa vizimba kukabiliana na upungufu wa samaki

Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara  Prof. Sospter Muhongo amesema,  kutokana na kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria Jimbo hilo limeweka malengo ya kuanzisha na kuendeleza uvuvi wa Vizimba katika kata 18 Kati ya 21 ambazo zina fursa nzuri ya kutumia rasilimali ya Maji ya Ziwa hilo kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi kwa Wananchi na Taifa pia.

Ameyasema hayo leo Februari 17, 2025, kupitia taarifa aliyoitoa kwa Wananchi wa Jimbo hilo.”Upungufu wa samaki haupo tu ndani ya Ziwa Victoria, bali ni tatizo kubwa ulimwenguni kote! Bahari, maziwa na mito ya Duniani kote ina upungufu mkubwa wa samaki. Kwa hiyo sasa takribani nusu (ca. 50 ) ya samaki duniani kote wanapatikana kupitia ufugaji wa samaki ndani ya bahari, maziwa nakadhalika (Acquireculture fish farming)”amesema Prof. Muhongo.

“Kata 18 kati ya Kata 21 za Jimbo letu zina ufukwe wa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, asilimia 85.7 (85.7%) za Kata zetu zina fursa nzuri za kutumia raslimali za maji ya Ziwa hili. Malengo yetu
ni kwamba Kata 18 kati ya 21 za Jimboni mwetu kuanzisha na kuendeleza Uvuvi wa Vizimba ndani ya Ziwa Victoria.”amesema Prof.muhongo.

Ameongeza kuwa, Mitaji ya Uvuvi wa Vizimba kupatikana kutoka kwa
Mitaji ya watu binafsi ambapo vizimba 10 vimeishaanza uzalishaji,
Pia,  Mitaji kutoka mikopo nafuu ya Serikali Kuu na vizimba 8 tayari vimetayarishwa na kuwekwa Ziwani. Na  Uzalishaji utaanza ndani ya miezi 3 ijayo.  Mitaji kutoka mikopo mizuri ya Benki za Biashara CRDB & NMB  Mikopo 10 ya vizimba 50 itatolewa hivi karibuni.

Pia Prof. Muhongo pia amesema,baadhi ya wavuvi wa vizimba wa Musoma Vijijini wamemueleza Mbunge huyo kuwa, kwenye kizimba kimoja chenye kipenyo cha mita 10 (10m-diameter) wamefanikiwa kuvuna tani 12 za samaki wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania  Mil.100.

Ameongeza kuwa,Uvuvi wa Vizimba ni njia nzuri na yenye mafanikio makubwa Sana katika kukuza kwa Kasi uchumi wa Jimbo la Musoma Vijijini na hivyo ametoa wito wadau mbalimbali wa Uvuvi kujitokeza kwenye Uvuvi wa kisasa ndani ya Ziwa Victoria. Ambalo amesema lina umri wa takribani miaka 400,000,  na ujazo wake wa kawaida ni kilomita za ujazo 2,760 (2,760 cubic kilometres).

Amebainisha kuwa,Mvua za mwaka jana ziliongeza ujazo wa maji ndani ya bonde la Ziwa Victoria lenye ukubwa kilomita za miraba 195,000 (195,000 square kilometres). Lilikuwa ongezeko la kina cha takribani mita 1.7 (ca. 1.7 meters depth).

Naye Shaban Majura Mkazi wa Kijiji cha Busekera Jimbo la Musoma Vijijini ameiambia kwa njia ya simu Majira Online kuwa , uvuvi wa Vizimba utaongeza manufaa makubwa ya kipato kwa wavuvi kuzalisha kwa tija na kulinda rasilimali zilizoko ndani ya ziwa Victoria kwa manufaa endelevu ya vizazi vya sasa na Vijavyo. 

“Tukizingatia Uvuvi wa Vizimba tutainuka kiuchumi. Tunaishukuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia amekuwa mstari wa mbele kusaidia Wavuvi tuvue   Kisasa na tuondokane na umaskini. Jambo hili linafaida kwa ukuaji wa uchumi wa Wavuvi na pia kipato cha Taifa letu.”amesema Masini Bwire anayejishughulisha na Uvuvi kata ya  Etaro Musoma Vijijini