January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge aiangukia Serikali isaidie wananchi waliokumbwa na mafuriko Kigoma

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Mjini Kirumbe Ng’enda (CCM) ameiomba Serikali kuitazama Kata ya Katubuka  ambayo imeathiriwa na mafuriko na hivyo kusababisha nyumba 80,nyumba za ibada ,kituo cha mafuta pamoja na miundombinu ya barabara kusombwa na maji.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu ambapo amesema barabara iliyoathiriwa na mafuriko ni ile ya kutoka Ulanga kelekea uwana wa Ndege wa Kigoma ambayo imefungwa kutokana na kuharibiwa na mafuriko..

“Kata ya Katubuka yametokea mafuriko makubwa ambayo yamesababisha zaidi ya nyumba 80 kuwa hazikaliki na kufanya makanisa mawili,kituo cha mafuta na barabara itokayo Ulanga kuelekea uwanja wa Ndege wa Kigoma kufungwa na kutokutumika jambo hili ni kubwa,na nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi ,

“Naiomba Serikali ,wakati inatazama maeneo mengine itazame na eneo hilo,hivi sasa Serikali ya mkoa ikiongozwa na mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishina Thobias Andengenye na mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kally wanaendelea kufanya kazi kubwa lakini wanahitaji msaada mkubwa wa ofisi ya Waziri mkuu kitengo cha maafa ili kuwanusuru wananchi kabla hali haijawa mbaya zaidi katika kata hiyo.”amesema Mbunge Ng’enda

Aidha amesema pamoja na kazi nzuri  ya Serikali kuna changamoto ya usimamizi hasa katika  ofisi ya Waziri Mkuu hali inayosababisha sekta binafsi kuchelewa kukua .

“Jambo hili halitupi furaha sisi wawakilishi wa wananchi ,suala  la sekta binafsi kuchelewa kukua linasababishwa na serikali kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya ulipaji wa madeni ya kazi ambazo zinafanywa na wakandarasi na wazabuni wanaotoa huduma kwa Serikali.”amesema Mbunge huyo

Amesema wakati mwingine sekta binafsi zinatoa huduma na kufanya kandarasi mbalimbali  za Serikali kwa kukopa fedha benki ambapo wanaendelea kudaiwa na riba  zinaendelea  kuongezeka na wala serikali haichukui hatua ya kulipa madeni yao kwa wakati.

Ng’enda amesema Serikali inapaswa ielewe kuwa sekta binafsi ndiyo nguzo ya uchumi wa Taifa hivyo inapochelewa kuwalipa inarudisha nyuma maendeleo ya sekta binafsi ,wananchi na Taifa kwa ujumla.