December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge afurahia kasi ya maendeleo Kaliua

Na Allan Vicent,TimesMajira Online, Kaliua

MBUNGE wa Jimbo la Kaliua Mkoani Tabora Aloyse Kwezi amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo hilo.

Akizungumza na gazeti hili juzi ameeleza kufurahishwa na miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na nishati ambayo imeleta tija kubwa kwa wananchi.

Alisema miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboreshwa kwa huduma za kijamii katika sekta hizo ikiwemo kuboresha mandhari ya mji huo ambapo sasa  hata wageni wanaotembelea wilaya hiyo wanatamani kuhamia hapo.

Alieleza kuwa kujengwa kwa hospitali ya wilaya, vituo vya afya, zahanati katika vijiji mbalimbali kumeongeza upatikanaji huduma za afya kwa wakazi wa wilaya hiyo tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Kwezi alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 2 ya utawala wa Rais Samia zaidi ya sh bil 60 zimepelekwa na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na kuboreshwa miundombinu ya afya.

‘Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha miundombinu na huduma za kijamii katika Jimbo hili na wilaya nzima, hakika Kaliua sasa inang’ara’, alisema.

Mbunge aliongeza kuwa awali hawakuwa na Mahakama ya Wilaya, Ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA), Ofisi ya Tanesco na Taasisi nyingine muhimu kwa ajili ya kuhudumia wananchi lakini sasa ujenzi umekamilika na huduma zinaendelea kutolewa.

Aidha alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa hamashauri hiyo kwa kuratibu na kusimamia kwa weledi mkubwa utekelezaji miradi ya maendele ikiwemo kasi kubwa ya ukusanyaji mapato, wilaya imeendelea kuwa kinara wa mapato katika Mkoa mzima.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua alisema atahakikisha fedha zote zinazoletwa na Mhesh Rais kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinasimamiwa ipasavyo na kufanya kazi iliyokusudiwa

Aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kuunga mkono dhamira njema ya Rais Samia na kutunza vizuri miradi yote inayotekelezwa na serikali ya awamu ya 6 ili idumu na kuwanufaisha zaidi

Picha ya Jengo la Utawala la Hospitali mpya ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora.