Na Mwandishi Wetu, Timesmajira online
HIFADHI ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuthibitisha hadhi yake ya kipekee duniani baada ya kutajwa kuwa hifadhi bora zaidi barani Afrika kwa kutembelewa na watalii.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Mei 05, 2025 na tovuti ya ‘Breaking Travel News’ ya nchini Uingereza, inayotoa taarifa kuhusu maendeleo katika sekta ya utalii duniani.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imeongoza kwenye orodha ya hifadhi kumi bora barani Afrika, ikiishinda Hifadhi ya Taifa Kruger iliyopo nchini Afrika Kusini iliyoshika nafasi ya pili, na Masai Mara ya Kenya iliyoshika nafasi ya tatu.

Ushindi huo unadhihirisha ubora wa Tanzania katika kuhifadhi maliasili na hivyo kuendeleza shughuli za utalii na uhifadhi endelevu.
Tukio la Uhamaji wa Nyumbu linalojumuisha zaidi ya Nyumbu milioni moja na nusu, Pundamilia na Swala wanaohama kila mwaka kwa ajili ya malisho linaendelea kuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka duniani kote.
Mbali na Uhamaji wa Nyumbu, Serengeti ni makazi ya wanyama wakubwa watano (The Big Five) kama Simba, Tembo, Chui, Faru na Nyati, pamoja na mamia ya spishi za ndege.
Kulingana na ripoti hiyo, orodha ya hifadhi bora haikuangazia tu mandhari ya kuvutia na urahisi wa kuona wanyamapori, bali pia juhudi za uhifadhi, ushirikishwaji wa jamii na mchango wa hifadhi hizo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kutajwa tena kwa Serengeti kama hifadhi bora barani Afrika ni ushahidi wa mafanikio ya kazi kubwa ya uhifadhi inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Taifa kwa ujumla.
Hifadhi nyingine zilizoorodheshwa katika kumi bora ni pamoja na Etosha (Namibia), Chobe (Botswana), Bwindi (Uganda), Volcanoes (Rwanda), South Luangwa (Zambia), Delta ya Okavango (Botswana), na Addo Elephant (Afrika Kusini).
Ushindi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti unakuja wakati Tanzania ikiendelea kuweka juhudi kubwa katika kukuza utalii kwa kupanua wigo kwa soko la kimataifa na kuhifadhi maliasili kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.



More Stories
Kikundi cha Mwanamke Shujaa chamchangia Fedha ya kuchukua Fomu Rais Samia
Magugu maji yatajwa changamoto ya uzalishaji umeme maporomoko Rusumo
Wataalam Maendeleo ya Jamii waaswa kutoruhusu tamaduni potofu