January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbowe ahitimisha awamu ya kwanza operesheni +255KatibaMpya

Na Lubango Mleka,Timesmajira online, Igunga.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)taifa Freeman Mbowe amewataka wananchi Wilaya ya Igunga kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kuwakomboa Watanzania na kuwatetea katika misingi minne inayo isimamia.

Mbowe amesema hayo katika uwanja wa Barafu wilayani Igunga alipofanya ziara ya kuhitimisha na kuitambulisha operesheni ya chama hicho ijulikanayo kwa jina la +255 Katiba Mpya iliyoanzia Kanda ya Magharibi.

“Ndugu zangu wa Igunga hii ni ziara yangu ya nane ya kuhitimisha operesheni yetu ya +255 katika mikoa ya Magharibi ya Kigoma, Rukwa, Katavi na Tabora,takribani miaka saba tumepita ya uvuli wa umauti, watanzania tulijaribiwa, tuliumizwa sana na tulionewa sana wapo watu ambao hawakufika leo hii kwa sababu ya watawala wa CCM hawakuamini demokrasia,” amesema Mbowe ameongeza kuwa

“Upinzani ulipoimalika katika nchi yetu ndipo vita kubwa iliibuka ya CCM, walipoamini kuwa hawawezi kuiba kura ndipo wakaamua kuiba uchaguzi wote, tutaendelea kusimama kama chama na kutetea wananchi ili wananchi wawe na sauti mbadala,”.

Aidha,amesema kuwa CHADEMA ni chama pekee cha upinzani kilichobakia ambacho kinapambana na CCM, hivyo amewataka wananchi kusimama na chama hicho kwa kuwa ndio mkombozi wa wananchi na watanzania kwa ujumla.

“Misingi minne ya CHADEMA ndiyo inayoifanya mioyo ya watanzania kujenga imani nayo,hivyo iteteeni kwa misingi hii, ya kwanza ni haki, tunaamini katika haki, hata maandiko matakatifu imeandikwa, na yanasema haki hulinyanyua taifa,hatutaki kuwa chama cha dhambi,”amesema Mbowe.

Amesema kuwa msingi wa pili ni uhuru, ambapo wanataka taifa la Tanzania watu wake wawe na uhuru wa mawazo,mikutano pamoja na uhuru wa kukutana, wa kufanyabiashara, kilimo na kujadiliana.

“Msingi wa tatu chama hiki kinaamini maendeleo ya watu, msingi wa viongozi kutokana na kura halali za watu, Tanzania tunafitinika kwa sababu tunapata viongozi walioingia madarakani kwa njia ya wizi, ukipita kote nchini viongozi wa vijiji na serikali hawawasomei mapato na matumizi wananchi wao kwa sababu walipita kwa wizi na dhuruma,”amesema Mbowe.

Msingi wa nne ambao CHADEMA unausimamia ni demokrasia, ambapo Mbowe amesema baada ya kuminywa kwa demokrasia vyama vingi vidogo vimekufa na kubakia vyama viwili tu vikubwa.

“Wamebakia Farasi wawili ambao ni CHADEMA na CCM, watu wa Igunga ninawaomba ambao mnaamini katika haki, uhuru wa watu, demokrasia, mnao amini katika maendeleo ya watu kipokeeni na kilindeni chama hiki msikipokee kwa ushabiki wa kuja mkutanoni na kuondoka, kama tunataka kuwaachia utawala bora watoto wetu ni lazima tulete utaratibu bora wa nchi yetu ndio tunataka tuupate kupitia katiba mpya,”amesema Mbowe.

Mbowe alimalizia kwa kusema kuwa, yapo mambo mengi CHADEMA inataka kuyafanya kwa kuanzia kurekebisha katiba ya nchi,tume ya uchaguzi na kuondoa sheria mbalimbali kandamizi.

Aidha amewaomba wananchi wa Igunga wasiiuwe CHADEMA kwa kuwapatia Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais, ambao ni viongozi wadilifu watakao leta furaha kwa wananchi wote.

Huku Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi Gaston Shundo Garubindi na Mbunge atakayegombea Jimbo la Igunga Mjini kupitia chama hicho Ngassa Ganju Mboje, wamewapongeza wananchi wa mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma na Tabora wanaounda Kanda ya Magharibi kwa kuwapokea kwa wingi jambo ambalo linawatia moyo kwani ni kwa miaka mingi wananchi walikuwa na hamu kubwa ya kusikiliza hoja za mabadiriko kutoka kwa viongozi wa CHADEMA.

“Mwenyekiti na wananchi hii ni Igunga na ni Jimbo la mwisho kuhitimisha ziara yetu kati ya majimbo 25 ya Kanda yetu ya Magharibi, kwa niaba ya viongozi wa kanda hii viongizi wa chama, naomba nikushukuru wewe Mwenyekiti na kamati kwa maamuzi ya busara kuanza operesheni ya +255 Kanda ya Magharibi,”amesema na kuongeza kuwa

“Hatukuwa na nguvu kiasi hicho ila mmeona mje tuunganishe nguvu kuiondoa CCM madarakani, wana wa Magharibi tuna kazi moja ya kuhakikisha ambayo Mwenyekiti umeifanya na viongozi wengine tunaiendeleza, Kanda ya Magharibi ikawe ndio mwisho wa uongozi wa CCM,”.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Grace Kenedy, wamewashukuru viongozi wa CHADEMA Taifa, Kanda ya Magharibi, Mkoa wa Tabora na wilaya ya Igunga kwa kuwakumbuka na kuhitimisha ziara hiyo ambayo imewapatia mwanga utakao wasaidia kujikomboa kifikra, kimaendeleo jambo ambalo litawasaidia kusimama pamoja na kudai Katiba Mpya, kubadirishwa kwa sheria kandamizi, kuwepo kwa uhuru ikiwa ni pamoja na uwajibikaji kwa viongozi.

Operesheni +255 Katiba Mpya imeanza kwa Kanda ya Magharibi katika mkoa wa Kigoma, Kigoma mijini Mei 17,2023 na kuhitimishwa tarehe Mei 29,2023 kwa awamu ya kwanza mkoani Tabora Igunga mjini.