Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MBIO za Urafiki zitakazoshirikisha wanariadha wa nchi za India na Tanzania zimezinduliwa rasmi Dar es Salaam jana.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 30 na 31, mwaka huu ambapo zitaanzia Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani kwa siku ya kwanza na siku ya pili zitaanzia Bagamoyo hadi Dar es Salaam huku zikiongozwa na mkongwe wa riadha kutoka India, Milind Soman.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Balozi wa India hapa nchini, Manoj Varma, amesema wamefanya uzinduzi huo na maandalizi ya mbio yameshaanza kufanyika na wakimbiaji watakimbia kilometa 120.
Amesema mbio hizo zitahusisha wakimbia ambao ni raia wa Tanzania na India na usaili umeshafunguliwa kwa njia ya mtandao huku zikitarajiwa kuhusisha wakimbiaji mbalimbali.
Amesema wameandaa mbio hizo kuhakikisha wanadumisha umoja uliopo kati ya nchi hizo mbili ikiwemo wanariadha mbalimbali kubadilishana mawazo.
Ameongeza Soman ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa mbio za riadha nchini India, atapata fursa ya kuzungumza na wanariadha mbalimbali kuhakikisha wanabadilishana uzoefu.
“Umoja wa India na Tanzania tumeandaa mbio za riadha ambazo zitafanyika kuanzia Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani na baadaye zitatoka Bagamoyo kurudi Dar es Salaam ambapo tutakimbia kilometa 120, pia tutakuwa na mkongwe Soman ambaye hivi sasa ni mkufunzi wa mchezo na msanii wa filamu nchini India,” amesema alisema Kaimu Balozi wa India nchini, Varma.
Naye Soman amesisitiza kwamba ameshafanya mbio kama hizo katika nchi mbalimbali na sasa ni zamu ya Tanzania na yupo tayari kukimbia.
“Ni fursa nzuri kwetu kutembelea Tanzania kuja kuiongoza timu itakayoshiriki mbio za riadha kwa pamoja ambapo tutaungana na Watanzania mbalimbali lengo ikiwa ni kubadilishana uzoefu.
“Nimeshafanya safari kama hizi katika nchi mbalimbali Ulimwenguni, sasa ni zamu ya Tanzania, kuhakikisha tunafikia malengo.
“Tunafurahi na tunajivunia kuwakilisha Ubalozi wa India nchini Tanzania kupitia mbio za riadha ninafikiri tutaacha alama kwa wenyeji,” amesema Soman
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania