December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbinu zahitajika kudhibiti watoto wa mitaani

Na Penina Malundo, timesmajira

SERIKALI na wadau mbalimbali wa masuala ya watoto nchini wameshauriwa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti wimbi la watoto wanaotoroka familia zao na kukimbilia mitaani,ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi changamoto zinazokabili watoto katika familia zao.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na migogoro inayojitokeza kati ya wazazi,hali inayowafanya watoto kukimbia majumbani mwao na kuishi mitaani,hali duni pamoja na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam,Ofisa Ulinzi na Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la Railway Children,Marry Mushi wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani inayofanyika Aprili 12 kila mwaka.

Amesema migogoro na mifarakano baina ya wazazi inayojitokeza ndani ya familia inachangia kwa kiasi kikubwa watoto wengi kuingia mitaani bila wao wenyewe kupenda kutokana na nyumba wanazoishi kutokuwa na amani.

Amesema kuna wakati migogoro hiyo inafanya wazazi kutengana na hapo watoto wanakuwa hawana usimamizi mzuri ndani ya nyumba na kuwafanya watoto kuamua kutoka na kuanza maisha ya mtaani.

”Mara nyingi tumekuwa tukifanya mazungumzo na watoto wanaoishi mitaani na pia uwa tunatembelea familia zao kabla ya kuwarudisha watoto hao majumbani mwao,hivyo watoto wengi wamekuwa wakisema sababu ya wao kukimbia nyumba zao na kuingia mtaani ni kutokana na mifarakano ya wazazi inapotokea,”alisema na kuongeza
”Utakuta wazazi wametengana alafu mtoto anakuwa hatakiwi upande wa Mama wa Kambo au Baba wa Kambo kwahiyo kunakuwa na mvutano na kumfanya mtoto kushindwa kusimamia wapi katika makuzi yake na kuamua kwenda kuishi mtaani,”amesema.

”Watoto hawa wanataja ukatili wa kijinsia nao ni chanzo cha wao kuishi mitaani na kukimbia familia zao majumbani kutokana na wao kufanyiwa ukatili wa kimwili ambao umekuwa ukiwaathiri kisaikolojia na kuamua kukimbia nyumbani na kuishi mtaani,”amesisitiza.

Amesema shirika lao limekuwa likishirikiana na afisa ustawi wa jamii,viongozi wa serikali za mitaa,watoto wenyewe na wazazi wao katika kuhakikisha wanawaelimisha watoto hao umuhimu wa kuishi nyumbani na familia zao kisha kuwarejesha katika familia zao.

Kwa Upande wake Meneja wa Shirika hilo,Rose Kagoro amesema katika kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita,shirika lao katika kuhudumia watoto kwa mwaka jana kuanzia Januari hadi Disemba shirika lao liliweza kuunganisha watoto 303 na familia zao.

”Shirika letu limesaidia watoto 337 kati yao wakike 137 na wakiume 200 kurudi shule na watoto 94 kuwapa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana ambapo kati yao wakiume ni 73 na wanawake ni 21 huku wazazi na walezi 217 nao tuliwapatiwa mafunzo ya malezi chanya kwa watoto wao,”amesema.

Aidha amesema watoto 164 waliweza kupatiwa malezi mbadala ya kifamilia kupitia watu wa kuaminika huku watoto 167 walisaidia kuwapatia msaada wa kisheria.

Kagoro amesema katika kuadhimisha siku hiyo ya watoto wa mtaani,shirika lao limeiomba Serikali kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum kushirikiana na wadau kuendesha kampeni za utoaji elimu kwa jamii kwa wale wanaofanya kazi na watoto wanaoishi mitaani kupunguza vitendo vya ukatili.