January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MBIBO: Sera ya madini nguzo muhimu kuimarisha sekta ya madini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Imeelezwa kuwa Sera ya Madini ya 2009 imekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha Sekta ya Madini, japokuwa kuna haja ya kuhuisha sera hiyo ili kuendana na mabadiliko ya sasa pamoja na matarajio ya baadaye katika maendeleo ya Sekta ya Madini na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa jana mkoaji Morogoro na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini,  Msafiri Mbibo wakati akiongoza Kikao cha Mapitio ya Sera ya Madini ya mwaka 2009, kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro na kuhudhuriwa Wataalam wa Sera, na Wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa lengo la kufanya mapitio ya Sera hiyo na kuandaa mapendekezo ya maboresho.

Alisema kuwa mchakato mapitio ya Sera ya Madini ya mwaka 2009 katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi nchini. 

“Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na Sera ya Madini inayoendana na viwango vya kitaifa na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kijamii. Tunahitaji sera itakayotoa mwongozo thabiti wa usimamizi endelevu wa rasilimali za madini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Mbibo.

Mbibo alisema  kuwa, Wizara ya Madini hivisasa inaongozwa na Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inalenga masuala mahsusi yakiwemo kuimarisha ushirikiano wa Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi; kuboresha mazingira ya kiuchumi kwa uwekezaji; kuongeza faida kutokana na uchimbaji madini; kuboresha masuala ya kisheria; kuendeleza wachimbaji wadogo; pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira.

Akitoa wasilisho kuhusu Manufaa ya Sera ya Madini 2009, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini,Angelo Haule, amesema kuwa, ukuaji wa Sekta ya Madini umeimarika na Mchango wake kwa Taifa umeongezeka ambako kati ya Machi 2021 na Mei 2024, Tume ya Madini ilikusanya shilingi trilioni 1.93 kama Mapato ya Serikali, ikionyesha ufanisi mkubwa wa usimamizi wa sekta hiyo.

“Ukuaji wa sekta uliongezeka kwa kiwango cha asilimia 7.3 hadi 10.9 kati ya mwaka 2020 na 2022, huku mchango wake kwenye Pato la Taifa ukiongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022. Aidha, masoko 42 na vituo 100 vya ununuzi wa madini vimeanzishwa, na kusaidia mauzo ya madini zenye thamani kubwa ikiwa ni pamoja na dhahabu, almasi, na tanzanite”amesema Haule

Haule alisisitiza kuwa, kwa upande wa ununuzi wa bidhaa na huduma, Kampuni za Kitanzania zilishiriki kwa asilimia 82 mwaka 2021 na asilimia 86 mwaka 2023, ikidhihirisha ongezeko la mchango wa wazawa kwenye sekta hiyo kwa kutoa huduma na kusambaza bidhaa migodini.

Ameongeza kuwa, zaidi ya leseni 23,924 za Uchimbaji Madini ya aina mbalimbali zilitolewa kati ya Mwaka 2021 na 2024, hatua inayolenga kuimarisha uwekezaji na ufanisi wa Sekta ya Madini nchini.