Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali imepongeza mchango wa Wajiolojia na Wajiosayansi katika kusaidia kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda nishati safi ikiwemo azma ya kutumia utajiri wa madini ya Tanzania kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Hayo yamebanishwa leo Desemba 4, 2024 jijini Tanga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo kwa niaba ya Waziri wa Madini wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wajiolojia nchini.
‘’Ni ukweli usiopingika kuwa rasilimali madini zilizogunduliwa Tanzania, rasilimali ya gesi asilia, gesi ya helium na rasilimali zingine ni matokeo ya utaalamu wa wanajiosayansi. Kwa hili tunawapongeza sana,’’ amesema Mbibo.
Ameongeza kwamba, Serikali imeendelea kutumia wanajiosayansi katika kufanya tafiti kwa lengo la kubaini uwepo wa madini nchini kupitia maono ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri na kueleza kwamba katika kufanikisha maono hayo, wanajiosayansi wameendelea kutumia utaalamu wao katika kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa lengo la kutambua tabia za miamba.
Ameeleza kwamba, Sekta ya Madini nchini imeendelea kuimarika na kufanya vizuri mwaka hadi mwaka huku ikiendelea kuchangia katika uchumi na mapato ya Serikali ikiwemo ongezeko la ajira za moja kwa moja kwa Watanzania ambapo zimefikia zaidi ya 16,000, huku nafasi za juu kwa baadhi ya miradi mikubwa zikiwa mikononi mwa watanzania.
Pia, Mbibo ameeleza kuhusu hatua mbalimbali za kimkakati zilizochukuliwa na Serikali zenye lengo la kuimarisha sekta ya madini nchini na kuzitaja baadhi kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini; utekelezaji wa ajenda ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi badala ya kusafirisha madini ghafi;
Amezitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya wachimbaji wadogo; utekelezaji wa programu mbalimbali za kama vile Mining for Brighter Tomorrow (MBT); na usimamizi makini wa utekelezaji wa Kanuni za Maudhui ya Ndani yaani Local Content.
Akizungumzia changamoto ya muda mrefu ya kutokuwepo kwa Bodi ya Usajili wa wanajiosayansi, inayoikabili Jumuiya ya Wanajiosayansi nchini, Mbibo amewataka kuendelea kuwa watulivu wakati Wizara kushirikiana na Uongozi wa Jumuiya wa Wajiolojia Tanzania inaendelea kulifanyia kazi suala hili.
Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘’kutumia utajiri wa madini ya Tanzania kwa mendeleo endelevu ya kiuchumi na kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda nishati safi’’.
More Stories
CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto