Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,
ALIYEKUWA Mgombea wa kiti cha ubunge jimbo la Biharamulo mwaka 2020 kupitia CHADEMA,Mwalim u Mbelwa Petro amekihama chama hicho leo Machi 25,2025 na kujiunga na CCM akipokelewa na kukabidhi kadi kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira akiwa mkoani Kagera.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa kiongozi huyo wa CCM kuifanya mkoani Kagera tangu aidhinishwe na chama hicho kushika wadhifa huo mnamo 18-19 Januari, 2025.
Mwanasiasa huyo kijana amesema kuwa CCM ni chama kilichokamilika kimfumo kwa ajili ya kuiongoza nchi kuleta maendeleo huku amani ikiwa ni kipaumbele cha kudumu.Mbelwa amesema kuwa chama chake cha awali CHADEMA bado kinajisuka huku kikiteswa na zimwi la uchanga, upendeleo, utovu wa nidhamu na mikakati isiyofanya kazi.
Mbelwa amesema “CHADEMA leo wanahubiri NO HATE, NO FEAR!, kesho wanahubiri JOIN THE CHAIN!, keshokutwa wanahubiri STRONGER TOGETHER!, mtondogoo wana NO REFORM, NO ELECTION, LEMA anawaimbisha tena wanachama TONE TONE, mara NIMO”, hakuna mkakati unaokamilika na kuleta matokeo kwa chama. Waswahili husema miruzi mingi hupoteza mbwa. Nimeamua kukihama chama hicho kwa hizo inconsistencies katika mikakati yake”
Kuhusu suala NO REFORM NO ELECTION, Mbelwa amesema CHADEMA imeibuka na mkakati huo kutokana na maandalizi hafifu ya kushiriki uchaguzi hivyo hiyo kauli inatumiwa kama kichaka cha kujifichia ili wasishiriki uchaguzi”.
Mbelwa aliongeza kwa kusema kuwa “kitendo kinachopangwa na CHADEMA cha kuzuia uchaguzi usifayike ni ndoto ya mchana kwa sura moja na ni uhaini kwa sura nyingine. Mimi siwezi kuoteshwa ndoto hizo na kamwe siwezi kuendelea kufikiria kufanya uhaini wa namna hiyo kwa nchi yangu, sikuwahi kuwa mwanasiasa mwenye malengo machafu kwa nchi yangu”.
Mbelwa amesema “ni vigumu kwa chama kilichoshindwa kuweka utulivu kwenye ofisi moja ya makao makuu iliyopo Mikocheni kuleta utulivu kwenye nchi yenye kilomita za mraba 945,000 na watu wake milioni 60”.
Ameongeza kuwa kutokana na mahaba waliyonayo Watanzania kwa CCM, ukipingana na CCM unajitakia taabu za maksudi pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo moyo kuvimba.
Amesema “Mimi Mbelwa Petro nimeona nitosheke na taabu nilizozipata kwa kuwa mwanaCHADEMA, sasa inatosha.”
“Mwaka 2020 nilipogombea ubunge jimbo la Biharamulo, nilipata shida za kujitakia na baada ya uchaguzi kuisha niliambulia kuitwa Mbunge wa wananchi, nikamuuliza Mh.Mbowe, sisi wabunge wa wananchi tutakwenda kuapia wapi? Akasema, atanijibu baadae. Hajanijibu mpaka leo tarehe 25 Machi, 2025.
“Nikamuacha nikaenda kwa Kaka Lissu kwa kuwa yeye ni mwanasheria, nikamuuliza vipi Mzee sisi wabunge wa wananchi tunaapa kwa katiba ipi? Ni lini? Na wapi?”.
Lissu akaniambia niwe mtulivu kwani naye yupo anatorokea Ubelgiji kutokana na hali kuwa ngumu. Nilichoka, na kupata taabu mara mbili”. Aliongeza.
Mbelwa alisema “nisiseme mengi, kwa sasa nawaomba wanaCCM mnipokee, kuanzia sasa nimeacha kukunjishwa ngumi pasipo kuwa na mtu wa kupigana naye”.
Kuhama kwa kada huyo linaweza kuwa pigo kwa CHADEMA jimbo la Biharamulo kwa kuwa mwanasiasa huyo alikuwa na ushawishi mkubwa hasa kwa vijana katika jimbo na mkoa mzima kwa ujumla.
More Stories
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.Â
Samamba:Uongezaji thamani madini ni mkakati wa serikali kukuza mchango wa sekta
Prof.Muhongo apongezwa kuleta majadiliano sekta ya elimu Musoma