Na Doreen Aloyce
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimefungua milango kwa chama chochote cha siasa nchini, ambacho kipo tayari kushirikiana nacho kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu katika uchaguzi mkuu 2020.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Alisisitiza kwamba katika uchaguzi mkuu mwaka huu chama hicho kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa maslahi ya taifa. “Niseme tu kwa moyo mmoja, sisi tupo tayari kushirikiana na chama chochote kile cha siasa kwa maslahi ya Mama Tanzania, kwani hata salamu yetu inasema kwa pamoja tutashinda,”amesema Mbatia
Mbatia pia amesema katika uchaguzi mkuu 2020, ajenda yao ni katiba mpya kwani ndiyo kauli ya umma wote. “Ajenda yetu katika uchaguzi huu ni Katiba mpya ni haki yetu kauli hii inatokana na umma wote lazima tutaendelea kuipigania kwa mslahi ya Taifa letu,”amesema Mbatia.
Akizungumzia kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini NEC, amesema kuwa inatakiwa kuzingatia taratibu za kisheria na kikanuni zinafuatwa na maamuzi yanatolewa kwa usawa na haki.
“Uchaguzi Oktoba tunataka kuliingiza Taifa hili katika historia mpya kwa Tume ya Uchaguzi kutenda haki na usawa,”amesema.
Wakati huo huo, Mbatia amesema chama hicho kitatoa ratiba ya uteuzi wa wagombea urais, wabunge, madiwani pamoja na wawakilishi, mwanzoni mwa wiki ijayo.
Mbatia amesema tayari ameshamwagiza Katibu mkuu wa chama hicho kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea ndani ya chama mapema wiki ijayo. “Nitoe wito kwa vijana na wale wote wenye sifa, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, katika uchaguzi huu, katika nafasi za urasi Tanzania Bara na Zanzibar, ubunge, wawakilishi pamoja na zile za udiwani,”alifafanua Mbatia.
Vilevile aliwapongeza watu waliojiunga na chama hicho hivi karibuni, wakiwemo wabunge na viongozi wengine wakubwa. Akizungumzia kuhusu mlipuko wa virusi vya Corona, Mbatia amesema kuwa wao kama chama cha siasa wanaendelea kuwatahadharisha wananchi kuendelea kuchukua hatua ili kujikinga.
“Corona bado ipo, tuendelee kuchukua tahadhari na kuondoa hofu mimi ni mtaalam wa majanga lazima tuhakikishe kuwa hofu yetu inaondoka kwani inachangia katika kushusha kinga ya mwili kwa kiwango kikubwa sana,”amesema
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa