January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na pingu na funguo zake

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na vifaa vya vya Jeshi hilo pamoja na Jeshi la Wananchi ambapo lengo lake ni kuvitumia kwenye matukio ya kiharifu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, ACP August Urio akitoa taarifa Januari 5,2024 kwa Waandishi wa Habari katika mahabusu ya Wilaya Mpanda amesema kuwa mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa watu 83 waliokamatwa kwa makosa mbalimbali kwa kipindi cha mwezi Desemba mwaka uliopita.

Urio amefafanua kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo akiwa na vifaa vya jeshi kama vile sare za Jeshi la Wananchi na Polisi, pingu zikiwa na funguo zake pamoja na mkanda ni matokeo bora ya doria na misako wanayoifanya kubaini,kuzuia na kutanzua uhalifu.

Kaimu kamanda huyo ameeleza katika msako huo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja akiwa na dawa za kulevya zinazo dhaniwa kuwa ni mirungi gramu tatu,watu nane wakiwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni bangi kg 4 na kete 90 pamoja na watuhumiwa 17 wakiwa na pombe haramu ya moshi kiasi cha lita 405.

Aidha watu 56 wanaojihusisha na matukio ya wizi,uporaji,uvunjaji na unyang’anyi wamekutwa wakiwa na vielelezo vya wizi zikiwemo pikipiki nne MC.456 BCS aina ya Fekoni,MC 861 DDR aina ya Kinglion, MC 104 DWL aina ya Sanlg na aina ya Sanlg isiyokuwa na namba.

“Tumewakamata pia na mbolea za ruzuku mifuko 48 kati ya hizo Npk mifuko 29,Can mifuko 11 na Urea mifuko 8,”amesema Urio.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limepata mafanikio ya kesi mahakamani ambapo watuhumiwa 108 wamefikishwa mahakamani ikiwa watuhumiwa 28 wamehukumiwa vifungo gerezani,watuhumiwa 26 wamehukumiwa kulipa faini,watuhumiwa 10 wameachiwa huru na 44 bado kesi zao zinaendelea mahakamani.

Vilevile Jeshi la Polisi linawaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi kuongeza ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa zitakazo saidia Mkoa kuendelea kuwa salama.