Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amewahakikishia wananchi wa Mbarali na Watanzania kwa ujumla kuwa zoezi la kuwarejesha wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo litakuwa endelevu na lenye kuleta tija na ufanisi kwa wananchi wanaokaa kandokando mwa Hifadhi ya Taifa Ruaha na Pori la Akiba Mpanga-Kipengele.
Kairuki ameyasema hayo Mei 09 mwaka huu, Wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya, alipokwenda kuzindua na kushiriki zoezi la kufukuza Tembo katika Kata tano za Igava, Mawindi, Miyombweni, Imalilosongwe na Rujewa ambazo ndio waathirika wakubwa wa wanyama hao.
Akiwa katika zoezi hilo aliwahakikishia wananchi hao na watanzania kwa ujumla kuwa zoezi hilo si la muda mfupi kwani litaleta tija kwa wakao wa maeneo hayo.
“Zoezi hili si la muda mfupi, ni matumaini yangu litaleta tija na ufanisi mkubwa kwa wananchi wetu, najua changamoto mliyokuwa nayo ndio maana Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imeamua kulishughulikia kwa haraka. Ndani ya muda mfupi mtaona mabadiliko makubwa,” amesema Kairuki.
Aidha, Kairuki aliongeza kuwa kwa siku mbili wataalam walifanikiwa kuwaswaga na kuwarudisha hifadhini takribani tembo 61, ambapo juzi makundi matano yenye tembo 43 na jana tembo 18 wamerejeshwa katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Ili kupunguza vifo visivyo vya lazima, Kairuki alisema Tembo ambao wanavamia maeneo ya wananchi wasijichukulie sheria mkononi kwa kuwaua
“Kwa kawaida tembo huwa ana tabia ya kulipiza kisasi, lazima mtambue kuwa hata ikipita miaka mingi tembo hasahau eneo alilouwawa mwenzao au alipopata kadhia na bughuza, akipita eneo hili na akakutana na binadamu lazima alete taharuki na kujueruhi,” amesema Kairuki.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo (Mb) aliishukuru Wizara na taasisi zake akisema, “Niwapongeze wataalam kutoka TANAPA, TAWA, TAWIRI na TFS kwa kufanya kazi usiku na mchana, matokeo yameonekana, hivyo wana Igava, Ikanutwa na maeneo mengine ambapo zoezi hili linafanyika tutapata ahueni”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi