Na Pius Ntiga, TimesMajira Online,Moshi
ZAIDI ya hekari 250 zinatumika katika uwekezaji wa Sh.Bilioni 6 tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 1,000 katika shamba la mwekezaji wa Maua la Vasso linalomilikiwa na raia wa Uholanzi, Fons Nijenhuis lililopo Kijiji cha Dakau Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyoahidi kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kama njia moja wapo ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akizungumza na Gazeti la Majira mwekezaji Fons Nijenhuis,amesema uwekezaji huo umetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na pia amesaidia kuchangamsha eneo kibiashara na hivyo kuinua uchumi.
Aidha,amesema amefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi wanozunguka shamba hilo ambao miongoni mwao wameanzisha kilimo cha maua ambayo huyauza kwake.
“Ngoja nikwambie hapa mimi nimefanikiwa kufundisha ujuzi wananchi wapo kama 40 hivi hawa wote wana mashamba hapo nje na maua yao huwa wananiuzia mimi na huwalipa kiasi cha milioni kama moja hivi kila wiki wanaponiuzia Maua” amesema.
Kwa mujibu wa mwekezaji huyo kila wiki husafirisha zaidi ya tani 250 za miche ya maua nje ya nchi na sehemu ya fedha zake hutumika pia kufanya ukarabati wa huduma katika vijiji vitatu vinavyozunguka Shamba hilo.
Katika shamba hilo amesema amekuwa akitunia tani 500 za udongo ambazo huziagiza kutoka nchini Uholanzi na kwamba udongo wa hapa nchini hautoshelezi.
Amesema anaendelea kufanya mazungumzo na Serikali ili kuangalia uwezekano wa kuwa anatumia udongo wa hapa nchini ambao unapatikana Wilayani Pangani mkoani Tanga lengo ni kuwezesha pesa anayotumia kuagiza nje udongo ibaki hapa hapa nchini Tanzania.
“Sehemu kubwa ya wateja wangu wapo nchini China na Uholanzi ambako huuza hii miche ya Maua” amesema mwekezaji.
Kwa upande wake,Afisa Kilimo Halmashauri ya Moshi Vijijini,Mercy Urio amesema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa jamii na Halmashauri ya Moshi vijijini na wananchi kwa ujumla na wanajivunia uwepo wa mwekezaji huyo.
Nao wanufaika wa uwekezaji huo,Agnes Shofa, Justina Mushi pamoja na Benard Erasto,wamesema kwa sasa maisha yao yamebadilika ukilinganisha na awali walivyokuwa, kwani wamefanikiwa kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba mpya.
Naye meneja wa shamba hilo Alany Njau,amevitaja vijiji vitatu vinavyonufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na kijiji cha Umbwe,Ucharo pamoja na Dakau na wamekuwa wakifundisha ujuzi kwa wananchi wa namna ya kupandikiza pia Vikonyo.
Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya ya Moshi Alhaj Rajab Kundya, aliambatana na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm,katika shamba hilo amesema mafanikio yote yamepatikana kutoka na uongozi thabiti wa Rais Dkt.John Magufuli na kusisitiza kuwa Chanda Chema huvikwa Pete.
Aidha,mkuu huyo wa Wilaya ya Moshi,amesema shamba hilo la Maua ni moja ya Mashamba 11 yaliyopo katika Wilaya hiyo limeendelezwa Vizuri kupitia pia vyama vya ushirika.
“Kuna changamoto kadhaa ambazo hujitokeza kwa mwekezaji huyo lakini tumekuwa tukikaa pamoja kuzitafutia ufumbuzi wa kina” amesema DC wa Moshi.
Amesema wanafarijika kuona maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha kutumia mvua kinapitwa na wakati na Serikali inahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa vizuri ili kuleta chachu katika kilimo cha umwagiliaji.
Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 /2025 imeahidi kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha biashara hususani ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea