Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Matawi 228 ya Benki ya NMB nchini katika kila eneo kupitia Mawakala wake zaidi 17,000 watasaidia kutoa huduma za ukadiriaji na kusanyaji kodi na tozo mbalimbali za ardhi nchini .
Hayo yamebainishwa tarehe 20 Desemba 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa uzinduzi wa mkakati maalum wa ushirikiano wa Wizara ya Ardhi na Benki ya NMB katika ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali za sekta ya ardhi uliofanyika jijini Dar es salaam.
Dkt Mabula alisema, mkakati wa kushirikiana na Benki ya NMB unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuandaa kampeni maalum ya ukusanyaji kodi na tozo mbalimbali za sekta ya ardhi ambapo wizara yake kupitia NMB na mawakala wao watatoa huduma ya ukadiriaji na ulipaji kodi ya ardhi kwenye matawi 228 ya Benki ya NMB katika kila eneo ambako mawakala zaidi ya 17,000 watatoa huduma.
Amesema, Wizara ya Ardhi tayari imetoa mafunzo ya namna ya ukadiriaji na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kwa wafanyakazi wa benki ya NMB kupitia njia ya mtandao ambapo matawi yote yalishiriki. Aidha, mafunzo kwa mawakala yamefanyika katika kila mkoa na zoezi linaendelea.
Amewataka wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo ya usogezaji huduma karibu na wananchi na ubunifu uliofanywa kwa kushirikiana na benki ya NMB.
Aidha, Waziri wa Ardhi katika uzinduzi wa kampeni hiyo aligusia pia suala la msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusiana na riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi ambapo wananchi walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili kusamehewa riba ya malimbikizo na nafuu hiyo ilitolewa kuanzia julai hadi desemba 2022.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, tangu msamaha huo utolewe takriban miezi mitano na nusu imepita na kasi ya wananchi kujitokeza bado hairidhisha ambapo Dkt Mabula alisema takwimu zinaonesha jumla ya wamiliki 2,819 ndiyo walioomba na kukidhi vigezo vya msamaha na shilingi 11,993,281,914 zililipwa kama deni la msingi.
Ametoa rai kwa wananchi wote kutumia kipindi hiki cha siku chache zilizobaki hadi desemba 31, 2022 kusheherekea siku kuu za mwisho wa mwaka kwa furaha ya msamaha wa riba baada ya kukamilisha kulipa deni la msingi ambapo amebainisha kuwa, baada ya muda huo ameelekeza ofisi zote za ardhi kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaodaiwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kukusanya maduhuli ya serikali.
‘’Ofisi haitasita kuchukua hatua za kuanza kufuta umiliki kwa waliokaidi kutimiza takwa la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha sheria ya ardhi (Sura 113) kwa yeyote mwenye kumiliki ardhi ana wajibu wa kutimiza masharti ya umiliki ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka na atakayeshindwa ameviunja sharti hilo na milki husika itabatilishwa’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB ambaye ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Bw. Filbert Mponzi alisema Benki yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha mkakati wa kusaidia ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi unafanikiwa na kuiwezesha serikali kukusanya mapato kupitia sekta ya ardhi.
‘’Benki yetu ya NMB imejipanga vizuri katika kuhakikisha mkakati huu unafanikiwa na Matawi yetu katika mikoa mbalimbali kupitia mawakala zaidi ya 17,000 nchini utawezesha kufanikisha mkakati huu wa kukusanya maduhuli ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali za ardhi’’ alisema Mponzi.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati