Na Dennis Gondwe, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amekabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili kwa shule zote zenye kidato cha tano na sita katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Msaada huo aliukabidhi kwa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika hafla fupi iliyofanyika katika viunga vya halmashauri hiyo eneo la Manispaa ya zamani.
Mbunge Mavunde amesema kuwa, vifaa alivyotoa vinalenga kuwahakikishia wanafunzi wa kidato cha sita wanakuwa salama katika kipindi chote watakachokuwa shuleni.
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia kazi, ajira na vijana aliwatakia heri wanafunzi wa kidato cha sita katika mitihani yao.
Alimuomba Mungu kuwawezesha wanafunzi hao kufanya vizuri na kufaulu vizuri mitihani yao.
Aidha, alimshukuru Rais wa Tanzania kwa uamuzi wake makini kuruhusu shule za kidato cha sita kufunguliwa.
“Napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli kwa uamuzi wake makini na madhubuti kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha sita wanarejea shuleni kuanzia leo (Juni Mosi) kujiandaa na mitihani yao ya kidato cha sita,”amesema Mavunde.
Vilevile, aliwashukuru wakuu wa idara ya elimu msingi na sekondari kwa ushirikiano mzuri wanaompatia kutekeleza majukumu yake.
“Ninajivua sana wakuu hawa wa idara kwa kazi nzuri wanayofanya katika Jiji la Dodoma. Nawashukuru pia wakuu wa shule na waratibu elimu kata kwa kazi nzuri wanayofanya,”amesisitiza Mavunde.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa mbunge huyo anafanya kazi kubwa kukuza sekta ya elimu.
“Napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini kwa kazi kubwa, amekuwa mstari wa mbele sana katika kukuza elimu. Mbunge huyu ni mpambanaji sana hivyo, ameona atoe vifaa vya kupambana na virusi vya corona katika shule zote 11 zilizopo katika Halmashauri ya Jiji ili wanafunzi wetu wawe salama,”alisema.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Maria De Mattias, Mwalimu Lowaeli Lyimo akiongea kwa niaba ya wakuu wa shule, alimshukuru Mbunge huyo kwa kuwa bega kwa bega na shule za serikali na binafsi katika halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Mbunge huyu amekuwa karibu sana na shule kwa kuzitembelea na kuongea na wanafunzi na kuwatia moyo katika masomo yao. Tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu kwa shule za jiji la Dodoma,”alisema Mwalimu Lyimo.
Vilevile, aliwashukuru maafisa elimu wa halmashauri kwa ushirikiano wanaoutoa kwa shule hizo na kuitaka jamii kuendelea kuwaombea wanafunzi hao waweze kufanya mitihani yao na kufaulu vizuri.
More Stories
Wajawazito 140, wapatiwa vifaa vya kujifungulia
Wasanii wazidi kumiminika JKCI ofa ya Rais Dkt. Samia
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo