January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde asikiliza kero za wachimbaji wadogo Lemishuku,Manyara

Na Mwandishi wetu 

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amefanya ziara kukagua shughuli za uchimbaji madini na kusikiliza changamoto za wachimbaji wadogo katika eneo la Lemishuku,Wilayani Simanjiro eneo ambalo ni maarufu kwa uchimbaji wa madini vito ya Green Garnet.

Waziri Mavunde amepata nafasi ya kukagua uwekezaji uliofanywa katika uchimbaji wa madini katika Kijiji cha Lemishuku na kuhaidi kuwa  Serikali itafanikisha urushwaji wa ndege nyuki (drone) katika eneo hilo kwa ajili ya utafiti wa kina ili kuwaongoza vizuri wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Akizungumza jana katika ziara yake ,Waziri Mavunde alisema ifikapo  mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 jengo la kituo cha ununuzi wa Madini litakuwa limekamilika ili kufanikisha urahisi wa biashara ya madini.

Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia  Hassan itatatuwa changamoto zote za Maji,Umeme,Barabara na Zahanati ili kuchochea shughuli za ukuaji wa sekta ya madini.

Mavunde  aliweza kuongoza  harambee ya zahanati ya Kijiji hicho  ambayo jumla ya matofali 4500,sarufi mifuko 183 na fedha Tsh 23m zimepatikana.

Awali akitoa salam Mbunge wa Simanjiro,  Christopher Ole Sendeka, alimshukuru Rais Dkt. Samia Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii katika eneo hilo la uchimbaji na kumshukuru Waziri Mavunde kwa kuwa Waziri wa kwanza kufika katika eneo hilo kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mh. Fakhi Lulandala aliwahakikishia wachimbaji wadogo wa eneo la Lemishuku kwamba Serikali ya ngazi ya Wilaya kupitia Taasisi mbalimbali zilizopo hapo zitahakikisha zinasimamia kwa ukaribu utekelezaji wa changamoto za wachimbaji ili kuweka mazingira mazuri ya uchimbaji katika eneo la Lemishuku.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo (FEMATA)John Bina na Mwenyekiti wa Mabroka Tanzania(CHAMATA) Jeremiah Kituyo waliipongeza serikali kupitia wizara ya madini kwa mipango ya uendelezaji wa sekta ya madini na kusisitiza kwamba wachimbaji wadogo kuzingatia sheria za nchi na pia kwa wafanyabiashara wa madini kuhakikisha wanakata Leseni ya biashara ya madini ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.