December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mauzo ya hisa JATU PLC yamefanyika kwa mafanikio

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online

KAMPUNI ya JATU (JATU PLC) imesema kuwa mauzo ya hisa kwa umma yamefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo hisa zipatazo 15,526,372 zimeuzwa kwa umma  ikilinganishwa na lengo la kuuza hisa 15,000,000.

Akizungumza hayo juzi Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Peter Gasaya wakati wa Mkutano mkuu wa wanahisa wa kampuni hiyo,alisema matokeo ya mauzo ya hisa za kampuni  hiyo  yamefanikiwa kwa asilimia  104.

Almesema mnamo mei 31,2021  mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)iliidhinisha maombi ya JATU PLC kuuza hisa 15,000,000 kwa umma kwenye soko la awali zenye  thamani ya Sh. Bilioni 7.5 kwa bei y ash.500 kwa kila  hisa.

Gasaya amesema mauzo ya hisa  hayo yalifunguliwa Juni 1,2021 na kufungwa Julai 15,2021.’’Uongozi wa JATU PLC unatoa shukrani za dhati kwa taasisi na wadau wote waliohusika katika mchakato wa kuwezesha mauzo ya hisa za kampuni ya JATU PLC kwa umma,ikiwa ni Pamoja na CMSA,Soko la hisa la Dar es Salaam(DES),’’alisema

Amesema kampuni yao inauhakika kwa sasa kuboresha miundombinu ya kilimo kwa kununua vifaa vingi na vya kisasa kama Trekta ,mashineza kuvunia na kulimia Pamoja na kujenga miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji na viwanda.

“Tunaamini ifikapo mwaka 2022 muda kama huu tutakuwa na ushuhuda mkubwa wa kusema kuhusu miradi ya kisasa ya umwagiliaji ambayo JATU sasa inaanza kujenga,”amesema

Aidha amesema kampuni yao inatarajia kuanzisha miradi mipya ya kilimo, kujitanua katika masoko na kuwa na matawi mengi zaidi ya kuwahudumia wanachama.


“Leo hii JATU tunasheherekea mafanikio kwa kutangaza mavuno ya mazao mawili yaani Mahindi na Mpunga ambayo yameonesha mafaniko makubwa kwa wingi wa mavuno, ubora na ushiriki mkubwa wa wanachama ukilinganisha na mavuno ya msimu uliopita wa mwaka 2019-2020,”amesema na kuongeza


“Kuna mabadiliko ya ratiba ambayo yamesababishwa na ukubwa na ubora wa uwekezaji wetu, kutokana na kuwa na ekari nyingi za kuhudumia na kwa kuzingatia kwamba tunahitaji kulima na kuvuna kwa kuzingatia ubora, Kampuni imeona ni vyema kuleta ratiba mpya ya kilimo kwa mazao mbalimbali kama itakavyoelekezwa katika Taarifa hii,”amesema

 
Gasaya amesema kutokana na ratiba hii wanatarajia mteja ambaye ni mkulima atapata fursa ya kupangilia ratiba na bajeti yake na kufanya maamuzi sahihi ya kushiriki katika miradi mbalimbali ya JATU kwani sasa miradi itafanyika kwa kupeana muda na hivyo kumfanya mkulima kuwa na nafasi ya kuwekeza na kuvuna angalau mara tatu (3) kwa mwaka kwa kushiriki mazao zaidi ya aina moja.


Alisema wanatambua ushiriki wa wakulima wadogo walioingia msimu huu wa 2021-2022 tunaruhusu wale wanaolima ekari 1 hadi 49 watalima kwa uwiano wa 1:50 yaani hisa hamsini kwa ekari moja, na kwa wale wakulima wote wanaolima ekari 50 na kuendelea watalima kwa uwiano wa 1:500 yaani hisa mia tano kwa ekari moja.